Nyie Man United sikieni bosi wa Spurs anavyosema

Sunday January 13 2019

 

LONDON, ENGLAND. MWENYEKITI wa Tottenham Hotspur, Daniel Levy amesema kamwe hawezi kukubali kumwachia Kocha Mauricio Pochettino aende akajiunge na Manchester United hata kama itawekwa mezani Pauni 50 milioni.

Bosi huyo wa Spurs amesema amewaambia wazi bodi kwamba hatakubali ofa yoyote ya kutoka Old Trafford itakayopelekwa kwao mwishoni mwa msimu ikilenga kumchukua kocha Pochettino.

Levy amewaambia marafiki zake na anampa heshima kubwa sana kocha huyo wa Kiargentina na kwamba hawezi kuthubutu kukubali kumpoteza.

Kocha Pochettino amekuwa akihusishwa na Man United kwenda kuinoa timu hiyo kabla ya hata Jose Mourinho hajafutwa kazi na baada ya tukio hilo kutokea mwezi uliopita basi jina la kocha huyo limetajwa zaidi huko Old Trafford.

Kwa sasa Man United ipo chini ya kocha wa muda, Ole Gunnar Solskjaer, lakini kilichopo ni kwamba ikifika mwisho wa msimu mambo yanaweza kuwa tofauti na wababe hao wa Old Trafford wakamteua kocha wao wa kudumu na kuachana na bosi huyo raia wa Norway, ambaye ana kibarua chake kinamsubiri huko Molde.

Man United ipo tayari kuwalipa Spurs Pauni 16 milioni kumnasa kocha huyo, lakini Levy amewakata kabisa maini akidai kwamba hata iletwe Pauni 50 milioni hawezi kukubali.

Advertisement