Nyie! Mwenye nyumba karudi kileleni

Muktasari:

Yanga imebakiza mechi mbili dhidi ya Mbeya City na Azam ambazo zote zitachezwa jijini huku Simba ikibakiza tano.

YANGA wamerudi kileleni baada ya matokeo ya jana Jumanne kuifunga Ruvu Shooting bao 1-0 hivyo, kuishusha Simba kwa pointi moja. Ushindi huo ni wa kwanza tangu Yanga ipate viongozi wapya wakiongozwa na Mwenyekiti, Dk Mshindo Msolla na makamu wake Fredrick Mwakalebela, ambaye alikuwa jukwaani akishuhudia mtanange mzima.

Yanga walifanya uchaguzi wake Mei 5, ambapo mechi ya kwanza ya viongozi hao kuishuhudia ilikuwa dhidi ya Lipuli FC kwenye nusu fainali ya Kombe la FA, ambapo walichapwa mabao 2-0 kisha kupoteza tena dhidi ya Biashara bao 1-0.

Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Uhuru, bao pekee la Yanga lilifungwa na Papy Tshishimbi na kuifanya kufikisha pointi 83 mbele ya Simba yenye 82.

Yanga imebakiza mechi mbili dhidi ya Mbeya City na Azam ambazo zote zitachezwa jijini huku Simba ikibakiza tano.

Tshishimbi alifunga bao hilo dakika ya 18 akitumia vizuri pasi ya Deus Kaseke na kuwaamsha mashabiki wa timu hiyo. Kipindi cha kwanza timu zote zilicheza kwa kushambuliana ingawa Ruvu Shooting walionekana kutumia zaidi mipira mirefu huku Yanga wakitumia krosi kupitia kwa Juma Abdul na Haji Mwinyi ambao, jana walikuwa bora zaidi kwa mipira ya krosi.

Yanga walionekana kusaka mabao ya haraka huku wakicheza mwa mipango zaidi, wakati Ruvu walikuwa wazuri tatizo ni kukosa mbinu za kuupenya ukuta wa Yanga uliokuwa chini ya Kelvin Yondani. Dakika 24 winga wa Ruvu Shooting, Emmanuel Martin alipiga shuti kali na kumbabatiza Yondani, hata hivyo kipa Klaus Kindoki aliudaka kwa umakini huku William Patrick akiwatoka wachezaji wa Yanga, lakini kazi nzuri ya kiungo Feisal Salum alikuwa kikwazo.

Katika mchezo huo, Yondani alipewa kadi ya njano kwa kudundisha mpira.

Dakika 31 Yanga walipigiana pasi za haraka haraka na kuingia ndani ya lango la Ruvu, ambapo kiungo Rafael Daud alipiga pasi ya mwisho kwa Herieter Makambo, ambaye akiwa hatua mbili na goli alipiga shuti juu la lango.

Hata hivyo, Makambo ambaye mabeki wa Ruvu walishindwa kumdhibit, alikosa nafasi nyingi za wazi, licha ya kutengenezewa pasi matata.

Mpaka kipindi cha kwanza kinaisha, Yanga ilikuwa mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili, Ruvu walibadilika na kulisakama lango la Yanga na dakika ya 49 walifanya mabadiliko kwa kumtoa Zuberi Dabi na kuingia Hamis Mcha.

Mabadiliko hayo yaliipa nguvu Ruvu baada ya Mcha kusukuma mashambulizi na dakika 53 shuti lake lilipanguliwa na Kindoki.

Yanga ilimtoa Abdul na Rafael na kuwaingiza Ibrahim Ajib na Thaban Kamusoko ili kuongeza nguvu.

Winga wa Ruvu, Patrick alionekana mwiba kwa Yanga akicheza vyema na Martin na kuwapa kazi ya ziada Yondani na Haji Mwinyi kuwazuia.

Hata hivyo, mpaka mwamuzi Hussein Athumani kutoka Katavi, anapuliza kipyenga cha mwisho, Yanga ilitoka uwanjani ikiwa kifua mbele.