Nyaraka za TRA zazua jambo kesi ya Aveva, Kaburu, Hanspoppe

Monday April 15 2019

 

By Fortune Francis

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga Aprili 29, mwaka huu kutoa uamuzi iwapo itapokea nyaraka za mamlaka ya mapato (TRA) kama kielelezo cha ushahidi katika kesi inayowakabili vigogo wa Simba, aliyekuwa Rais wa klabu hiyo,  Evans Aveva,  Makamu wa wake,  Geofrey Nyange na Mwenyekiti wa  Kamati ya Usajili wa Simba, Zacharia Hans Pope.

Uamuzi huo umefikiwa leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomasi Simba baada ya Wakili wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) Leonard Swai kuwasilisha hoja za upande mashta za kutaka nyaraka hizo zipokelewe kama kielelezo.

Aprili 10, 2019 upande wa utetezi ukiongozwa na Nehemia Nkoko ulipinga nyaraka zilizotolewa shahidi wa nne kutoka Mamlaka ya Mapato (TRA) shahidi anayetakiwa kueleza ni yule aliezitoa nyaraka hizo kwenye mfumo wa kompyuta.

Nkoko alidai nyaraka zinazotaka kutolewa ni za umma anayetakiwa kuzileta Mahakamani lazima azihakiki kwa kuweka tarehe jina na sahihi yake.

Swai alidai Mahakamani hapo anaomba nyaraka hizo zipokelewe kama kielelezo kwa kuwa nyaraka zilikidhi matakwa ya sheria ya ushahidi kwa mujibu wa kifungu cha 85.

Alidai sheria hiyo inamuelekeza kutoa nyaraka kwa kufuata taratibu ikiwemo kuweka tarehe, kuandika majina, cheo na kuweka sahihi.

Alidai kuwa kifungu cha 82(2) kinasisitiza Afisa lazima awe mtunza nyaraka na kufanya yote hayo tayari yeye ni mtunza nyaraka ambapo shahidi alielezea matendo yaliyopo kwenye sheria ya kuzitambua na kuelezea ufahamu wake.

Swai alidai Shahidi alielezea barua aliyoipokea kutoka Takukuru kwenda TRA ya tarehe 19,12,2017 wakiomba kujua ni kiasi gani cha fedha kilicholipwa.

Aliendelea kudai nyaraka zilizoambatanishwa ni stakabadhi za malipo ambazo sio lazima zitoke kwenye mfumo wa kieletroniki ni pamoja na barua ya TRA kwenda Takukuru ikielezea kiasi cha kodi.

Swai aliendelea kudai nyaraka nyingine hazikuwepo kwenye mfumo wa kieletroniki ni pamoja na maelezo aliyochukuliwa Amosi Juma ambayo yaliandikwa.

Baada ya kueleza hayo Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 29 mwaka huu kwaajiili ya kutolea uamuzi.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 10 ikiwemo kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi, kutoa maelezo ya uongo na utakatishaji wa fedha.

Katika shitaka la utakatishaji fedha linalomkabili Aveva, inadaiwa Machi 15, 2016 katika benki ya Baclays Mikocheni, Dar es Salaam alijipatia Dola za Kimarekani 187,817, takriban Sh. Milioni 400 kutoka katika Timu ya Simba wakati akijua zimetokana na zao la kosa la kughushi.

Katika shitaka la kughushi linawakabili washtakiwa wote, ambapo wanadaiwa katika tarehe hizo hizo kwa pamoja walighushi hati ya malipo ya kibiashara ya Mei 28, 2016 wakionyesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zinathamani ya dola 40,577 sawa na zaidi ya Sh. Milioni 90 huku wakijua kwamba sio kweli.

Pia katika shtaka lingine inadaiwa Aveva, Nyange na Hans Poppe kati ya Machi10 na September 30, 2016 waliwasilisha nyaraka za uongo kuonyesha Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,577.

 

Advertisement