Nusu fainali ya kibabe, kisasi FA Cup

Muktasari:

Arsenal ndio mabingwa wa kihistoria wa mashindano ya Kombe la FA wakiwa wametwaa taji hilo mara 13.

Newcastle,London. Vigogo vinne vya England, Manchester United, Arsenal, Manchester City na Chelsea vitakutana katika hatua ya nusu fainali ya Kombe la FA itakayochezwa kati ya Julai 18 na 19 kwenye Uwanja wa Wembley
Ushindi wa timu hizo katika mechi zilizochezwa juzi na jana umezifanya zikutane katika hatua ya nusu fainali ambayo inatazamwa kama nyakati nzuri ya kulipa kisasi kwa baadhi ya timu huku nyingine zikitaka kuitumia kuendeleza ubabe.
Katika droo ya hatua ya nusu fainali iliyochezeshwa jana kwenye uwanja wa St. James Park, Chelsea iliyoibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Leicester City imepangwa kukutana na Manchester United iliyoshinda mabao 2-1 mbele ya Norwich.
Chelsea licha ya kiu ya kutaka kuingia hatua ya fainali, mechi hiyo dhidi ya United pia ni fursa muhimu kwake kulipiza kisasi baada ya kuchapwa mechi tatu msimu huu na Manchester United.
United ilipata ushindi wa mabao 4-0 katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya England msimu huu dhidi ya Chelsea, ikaibuka na ushindi wa mabao 2-1 kwenye mashindano ya kombe la Calabao na pia ikashinda mabao 2-0 katika mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.
Lakini pia mechi nyingine ya hatua ya nusu fainali itakuwa ni baina ya Manchester City iliyoibuka na ushindi wa maba0 2-0 dhidi ya Newcastle jana dhidi ya Arsenal ambayo ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Sheffield United.
Baada ya kutandikwa mechi mbili za Ligi Kuu msimu huu dhidi ya Manchester City, itakuwa ni fursa muhimu kwa Arsenal kulipa kisasi mbele ya City ambayo imekuwa mbabe wao kwa muda mrefu.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amewataka wachezaji wake kuhakikisha wanakuwa mabingwa wa mashindano hayo kama njia pekee ya kuwapeleka katika mashindano ya Ulaya.
"Ni fursa kubwa kujaribu kushinda na kucheza katika mashindano ya Ulaya," alisema Arteta.