Nuno akitua Arsenal itakuwa vita ya dunia

Muktasari:

Mabosi wa Arsenal wenyewe wamemtimua Emery na kumleta Arteta wakiwa na ndoto za kumaliza msimu ndani ya Top Four ili kurejea kwenye mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada kushindwa kufanya hivyo kwa misimu kadhaa mfululizo.

LONDON, ENGLAND. ARSENAL mpo? Nafasi ya 10 kwenye msimamo baada ya kukusanya pointi 31 kwenye mechi 25. Imeshinda mechi sita tu msimu huu kwenye Ligi Kuu England, sare 13 na vichapo sita, imefunga mabao 32 na kufungwa 34. Kwa kifupi hali si nzuri kabisa.

Tangu ilipomfuta kazi Unai Emery, makocha wawili waliofuatia kuinoa timu hiyo, Freddie Ljungberg na Mikel Arteta wameshinda mechi mbili tu, moja kwa kila mmoja. Hali ni mbaya. Kwa pointi zake 31 inazomiliki, ipo juu kwa pointi saba tu kuzifikia timu zinazopambana zisishuke daraja, West Ham United na Watford zenye pointi 24 kila moja kwenye nafasi ya 18 na 19.

Mabosi wa Arsenal wenyewe wamemtimua Emery na kumleta Arteta wakiwa na ndoto za kumaliza msimu ndani ya Top Four ili kurejea kwenye mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada kushindwa kufanya hivyo kwa misimu kadhaa mfululizo.

Chelsea iliyopo Top Four, imekusanya pointi 41, pointi 10 zaidi ya zile inazomiliki Arsenal. Kwa maana hiyo, lugha nyepesi ni Arsenal kwa pointi zake ilizokusanya ni rahisi kushuka daraja kuliko kuikamatia Top Four. Mechi zake tano zijazo Arsenal Ligi Kuu England itacheza na Newcastle United uwanjani Emirates, kisha Everton hapohapo na baadaye itatoka kwenda Etihad kuikabili Manchester City kabla ya kurudi Emirates kucheza na West Ham United na itakwenda Brighton.

Kuona ugumu huo, tayari miamba hiyo ya Emirates imeshaanza kuhusishwa na mpango wa kumchukua kocha mpya. Nuno Espirito Santo wa Wolves anatajwa kwenye mpango huenda akaenda kuchukua mikoba huko Emirates.

Kocha huyo ambaye ni kipenzi cha mashabiki huko Molineux, mkataba wake umebakiza miezi 15 na hana mpango wa kusajili dili jingine jambo linaloishawishi Arsenal kufikiria kwenda kunasa huduma yake. Huko nyuma aliwahi kuhusishwa na Arsenal kabla ya kazi hiyo kupewa Arteta baada ya Emery kufutwa kazi Desemba mwaka jana.

Nuno aliulizwa kama mabosi wa Wolves wamempa ofa ya mkataba mpya, alisema: “Hawajanipa. Wala hakuna mpango huo. Bado kuna muda unaozidi mwaka mmoja hivyo sidhani kama kuna haraka ya kufanya hivyo.”

Wolves ya Nuno imekusanya pointi 35 katika mechi 25 ilizocheza, ikishinda nane, sare 11 na vichapo sita, huku ikifunga mabao 35 na kufungwa 32. Usiku wa jana Ijumaa ilitarajia kuwakabili Leicester.