Nsajigwa aipigia hesabu kali Kagera

Muktasari:

Ni mchezo wa Ligi Kuu utakaochezwa kwenye uwanja wa Kaitaba ambapo Kocha Msaidizi wa Singida United Shadrack Nsajigwa amesema hakuna kingine wanachokitaka zaidi ya kupata pointi tatu


Mwanza. BAADA ya kupoteza mchezo wao uliopita, Kocha Msaidizi wa Singida United, Shadrack Nsajigwa amesema kwa sasa akili na nguvu zao wanazielekeza katika mechi ijayo dhidi ya Kagera Sugar utakaopigwa kesho Jumatano mjini Bukoba.

Singida United ilichezea kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Alliance, ambapo na kesho itakuwa kibaruani tena kupepetana na Kagera Sugar ambao nao wametoka kuchezea kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Azam FC.

Nsajigwa alisema kuwa makosa ya kiufundi yaliyoonekana atayarekebisha kuhakikisha wanashinda mchezo huo na kuongeza kuwa wanaamini watashinda.

Aliongeza kuwa lengo lao ilikuwa ni kuondoka na pointi sita kwenye mechi mbili za Kanda ya Ziwa, lakini kutokana na kupoteza mchezo wa awali sasa wanazivutia kasi alama tatu kwenye mechi yao na Kagera Sugar.

“Tulihitaji kushinda michezo yote lakini ndio hivyo tulipoteza mechi na Alliance kwahiyo mipango yetu ni kupambana na alama tatu zilizobaki” alisema Nsajigwa.

Kwa upande wake Winga, Awesu Awesu alisema kuwa wanaenda kupambana kufa na kupona kuhakikisha wanashinda mchezo huo na kujiweka katika nafasi nzuri na kwamba yaliyopita hawayafikirii tena.

Alisema kuwa kikubwa ni kila mmoja kupambana kadri ya uwezo wake ili kuisaidia timu kuweza kupata pointi tatu na kwamba Kagera Sugar siyo timu ya kubeza hivyo inahitaji kwenda umejipanga.

“Tunajua mchezo utakuwa mgumu kutokana na wapinzani wetu kuwa wazuri, lakini tutapambana kadri ya uwezo wetu kuhakikisha tunashinda na kujiweka nafasi nzuri”alisema nyota huyo.