Nsajigwa: Ni vita ya Kapombe, Abdul

Muktasari:

Abdul amesema, ubora wake umeonakana kutokana na kujituma na kushirikiana na wachezaji wenzake: “Kila kitu ni malengo na kujituma.”

KWA mujibu wa beki aliyestaafu kwa heshima kubwa ndani ya Yanga na Taifa Stars, mabeki wa kulia, Juma Abdul wa Yanga na Shomari Kapombe wa Simba ni wachezaji bora mpaka sasa.

Wachezaji hao wote ni wenyeji wa Morogoro. Nsajigwa maarufu kama ‘Fusso’, amewataja Abdul na Kapombe ni miongoni mwa wachezaji wanaoitendea vizuri nafasi hiyo ya beki wa kulia.

“Ubora wa sifa ya beki mzuri wa kisasa wa pembeni hasa kulia ni yule mwenye uwezo wa kukaba na kushambulia. Awe na kasi na kufika sehemu husika kwa wakati,” alisema Nsajigwa ambaye kwa sasa anafanya ishu zake za ujasiriamali.

“Kwangu mimi Kapombe (pichani) na Abdul ambaye kwa sasa amerudi akitoka kwenye majeruhi wanafanya vizuri sana na sifa zote wanazo. Wachezaji wengine ambao wanafanya vizuri kikubwa wapambane zaidi yule Polisi Tanzania (William Lucian), Tanzania Prisons (Michael Ismail ) na yule wa Namungo (Miza Christom) hata Boxer (Paul Godfrey) wameanza vizuri,”alisema Nsajigwa ambaye aliwahi kuwa askari Magereza.

Kocha wa zamani wa Yanga, Kennedy Mwaisabula alisherehesha kauli ya Nsajingwa kwa kusema; “Namba mbili anayefanya vizuri kwa sasa kwangu ni Kapombe na Abdul baada ya kurudi kwenye kiwango chake anafuata. Wanaijua kazi yao na ndio maana wamekuwa msaada kwenye timu zao kwa sasa.”

Abdul amesema, ubora wake umeonakana kutokana na kujituma na kushirikiana na wachezaji wenzake: “Kila kitu ni malengo na kujituma.”

Kapombe amesema, ushirikiano kutoka kwa wachezaji wenzake na kuaminiwa na benchi la ufundi ndio umemfanya kufikia alipo sasa.