Nkana yanogewa na Hassan Kessy

Muktasari:

  • Kessy alikuwa kivutio kwa staili yake ileile ya uchezaji ya kupanda na kushuka huku akitumika kupiga krosi za maana zilizokuwa zikiipa presha Simba kwenye mchezo huo katika eneo lao la kujilinda.

VIGOGO wa Nkana FC ya Zambia, wameanza kuhusishwa kujiandaa kufanya mazungumzo ya kumuongeza mkataba beki wao Mtanzania, Hassan Kessy ambaye aliuwasha moto kwenye mchezo wa raundi ya kwanza dhidi ya timu yake ya zamani, Simba.

Moja ya mitandao ya kuaminika ya Zambia imeandika vigogo wa timu hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti Evaristo Kabila wamekuwa na mazungumzo ya siri ili kumfunga kitanzi beki huyo.

Kessy alijiunga na Nkana yenye maskani yake Kitwe, Zambia kwa kusaini mkataba wa miezi sita, baada ya Yanga kugoma kumpa mkataba mpya, Julai mwaka huu.

Beki huyo wa kulia alikuwa mmoja kati ya wachezaji muhimu wa Nkana waliofanya vizuri kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika mbele ya Simba ambayo ilipoteza kwa mabao 2-1.

Kessy alikuwa kivutio kwa staili yake ileile ya uchezaji ya kupanda na kushuka huku akitumika kupiga krosi za maana zilizokuwa zikiipa presha Simba kwenye mchezo huo katika eneo lao la kujilinda.

Moja ya krosi yake mwanzoni mwa kipindi cha kwanza iliunganishwa kwa kichwa na mshambuliaji wa Nkana, Ronald Kampamba na kugonga nguzo ya goli la Aishi Manula.

Mabao kwenye mchezo huo kwa upande wa Nkana yalifungwa na Ronald Kampamba na Mubanga Kampamba huku mahodha wa Simba, John Bocco akiwa mfungaji wa bao la timu yake.

YANGA WAMSUBIRI KESSY DAR

Simba inatakiwa kujiandaa kisaikolojia maana tayari Wazambia wameanza kuchapisha taarifa kuwa wanaweza kuwa kwenye nafasi nzuri ya kupata matokeo jijini Dar es Salaam kutokana na moja ya mchezaji wao kutokea Yanga.

Wazambia wanatambua kuna uhasama baina ya Simba na Yanga na kwa vyovyote vile timu hizo haziwezi kuwa kitu kimoja hasa upande wa mashabiki hata inapotokea timu moja inashiriki michuano ya kimataifa.

Hilo limeanza kujitokeza kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii ambayo imeanza kutumika kumkaribisha nyumbani Kessy na Nkana yake.

Mchezo wa marudiano kati ya Simba na Nkana utachezwa Desemba 23 na mshindi wa jumla ataingia hatua ya makundi.