Nkana ya Kessy yaaga mashindano Kombe la Shirikisho Afrika

Muktasari:

  • Kessy tangu ametua katika kikosi cha Nkana amekuwa na mafanikio makubwa pamoja na kujihakikishia namba ya kudumu kwa miamba hiyo ya Zambia

Tunis, Tunisia. Safari ya Tanzania katika mashindano ya klabu barani Afrika imefikia tamati jana baada ya beki Hassan Ramadhan ‘Kessy’ kushindwa kuisaidia timu yake ya Nkana ya Zambia kufuzu kwa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Nkana ilikubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Sfaxien katika mchezo wa marudiano uliochezwa kwenye Uwanja wa Taieb Mhiri jana Jumapili.

Matokeo hayo yanamfanya Kessyna Nkana yake kuaga mashindano kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya mchezo kwanza kuwafunga Sfaxien kwa bao 1-0 mjini Kitwe.

Kutolewa kwa Kessy imekuja siku moja baada ya wawakilishi wa Tanzania, Simba kuondolewa katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa baada ya kufungwa 4-1 na TP Mazembe.

Sfaxien iliingia katika mchezo huo  kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya saba lililofungwa na Firas Chaouat na kufanya timu hizo kwenda mapumziko matokeo ya jumla yakiwa 1-1.

Wenyeji waliendelea kulishambulia lango la Nkana, lakini washambuliaji wake walikosa umakini katika umaliziaji.

Katika kipindi cha pili, Nkana ilitawala mchezo kwa kumiliki mpira, lakini pasi zao za mwisho hazikuwa na macho.

Wakati mpira ukielekea mwishoni katika dakika 90, wenyeji Sfaxien walipata bao la ushindi lililofungwa na Alaa Marzouki kufanya matokeo kuwa 2-0 (Jumla 2-1) na kuamsha shangwe kwa mashabiki wao waliojitokeza Uwanjani.

Timu:

Sfaxien: Dahmen, Dagdoug, Sokari, Jelassi, Marzouki, Oueslati, Amamou, Mathlouthi, Zouaghi (Jouini 57’), Chaouat, Korichi (Harzi 70’).

Nkana: Malnga, Zulu (Masumbuko 68’), Nyondo, Bahn, Musonda, Kessy, Otieno, Musonda (Bwalya 83’), Malambo, K Kampamba, R Kampamba.