Njoo na kitochi chako Taifa, lazima Sudan wakae

KESHO Jumapili, Taifa Stars itaikaribisha Sudan uwanja wa Taifa ikiwa ni mechi ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi ya ndani huku waandishi wa habari na wadau mbalimbali wakijitokeza kuhamasisha kuishangilia timu hiyo kwa lengo la kuwapa nguvu wachezaji.
Habari njema ni kwama kamati hiyo ina tiketi kibao ya kukufanya shabiki ufike pale kwa Mkapa kuwapa nguvu wachezaji wa Stars, ni vipi utapata ni kupitia Mwanaspoti na vyombo vingine vya habari.
Kamati ya hiari inayoundwa na waandishi wa habari za michezo wameungana kwa pamoja na kamati zingine zilizo chini ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) kuhamasisha mashabiki kufika uwanjani kuwasapoti wachezaji wa timu hiyo inayoiwakilisha nchi.
Kamati hiyo ambayo ilianza harakati zake hivi karibuni kwa lengo moja tu la kuisapoti Taifa Stars leo Jumamosi ilitika ofisi za Mwananchi Communications Limited wachapishani wa magazeti ya Mwanaspoti, Mwananchi na The Citizens kuuelezea umma umuhimu wa mashabiki kuujaza uwanja wa Taifa ili timu yao ifanye vizuri.
Wajumbe wa kamati hiyo, Ally Kamwe na Karim Boimanda walisema kikubwa kinachopaswa kufanywa na Watanzania ni kwenda uwanja wa Taifa wakiwa na simu zao kwa lengo la kuishangilia Taifa Stars kwa namna ya kipekee.
"Tuliweza dhidi ya Burundi ambapo ulikuwa mchezo wa kuwania nafasi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia, hatuwezi kushindwa mbele ya Sudan, mashabiki walijitokeza kwa wingi kuisapoti timu yetu.
"Burundi nadhani walienda kusimulia kwao, ziliwashwa taa za tochi, naamini mchezo wakesho itakuwa mara mbili yake, nia na lengo lipo la kuing'oa Sudan," alisema Kamwe.
Kwa upande wa Boimanda aliishukuru TFF kutambua umuhimu wa mashabiki kuishangilia wa Taifa Stars na kuamua kuweka viingilio vya chini ili kila mmoja amudu kuisapoti Stars.
"Hakuna sababu ya kukaa nyumbani na kuungalia mpira kwenye televisheni, kwanini uishie kupiga kelele ukiwa nyumbani, nawaomba Watanzania wenzangu tukaujaze uwanja," alisema mjumbe hiyo.
Wajumbe hao walikabidhi tiketi 20 kwa ajili ya mashabiki watakaoingia uwanjani kuishangilia Stars ambazo zitagawiwa na Mwanaspoti ingawa haimzuii shabiki kununua tiketi na kwenda uwanjani bali anaweza kupata tiketi hiyo na kumnunulia mwingine tiketi nyingine ya kwenda kuisapoti timu.