Niyonzima awakumbuka Wakongo wa AS Vita

Muktasari:

  • Niyonzima ni mmoja ya wachezaji kutoka nje ya nchi waliokaa kwa muda mrefu hapa Tanzania tangu mwaka 2012 alipojiunga na Yanga na hivi sasa akiichezea Simba.

Kiungo wa Simba Haruna Niyonzima amesema 16 Machi itabaki kuwa siku kubwa kwake, huku akimshukuru kocha wake Mbelgiji Patrick Aussems kwa kumuamini na kumpa nafasi ya kucheza siku hiyo na kuisaidia timu yake kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya As Vita ya Congo.

Simba iliifunga AS Vita na kutinga moja kwa moja robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuwa timu pekee kutoka Afrika Mashariki kufika hatua hiyo msimu huu.

Kiungo huyo ambaye amekuwa hana wakati mzuri Simba kutokana na kuandamwa na majeruhi na wakati mwingine kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara,Jumamosi iliyopita aliingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya mshambuliaji Emmanel Okwi huku  akionyesha kiwango bora kilichowaduwaza mashabiki wengi waliokwe uwanjani na hata waliofuatilia mpira kupitia television.

Niyonzima alicheza kwa kiwango bora katika dakika chache alizopata nafasi ya kucheza mchezo huo na kuifanya Simba icheze soka la haraka na kushambulia hivyo kufanikiwa kupata bao la pili na la ushindi lililofungwa na kiungo mzambia Clatous Chama.

Mchezaji huyo raia wa Rwanda ameandika katika mtandao wake wa kijamii wa Instagram kuwa  licha ya kujisikia maumivu makali ya kifundo cha mguu dakika chache  tu tangu alipokanyaga nyasi za uwanja wa Taifa  lakini alipiga moyo konde kwani aliamini malengo yake ya kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika yasingetimia kama angeamua kutoka kutokana na maumivu hayo.

"16 Marchi ilikuwa siku kubwa katika maisha yangu soka ndani ya klabu yangu. Namshukuru kocha  kwa kuniamini  lakini dakika chache baada ya kuingia ndani ya uwanja nilijisikia maumivu mabaya ya  kifundo cha mguu lakini nilijiambia sitaruhusu hilo linitoe nje ya uwanja.

"Nilisema nimekuwa najitahidi katika mazoezi kwa kipindi kama hiki. Hii ni ndoto yangu  kama mtoto kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika hivyo hakuna chochote kitanisimamisha na sitaweza kuwaangusha mashabiki wa Simba,mamilioni ya watanzania na taifa langu pendwa la Rwanda.

"Hivyo nilijiambia nitacheza kwa moyo wote na sitacheza  na mwili wakati moyo wangu una nguvu na sasa tumetinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Inshallah  tutacheza fainali kwa sababu tuna kikosi cha kufanya hivyo na mashabiki wetu kamwe hawataacha kutuunga mkono," aliandika Niyonzima.