Niyonzima: Uvumilivu siri ya mafanikio yangu soka la Bongo

Muktasari:

Niyonzima amekuwa katika kiwango bora mwishoni mwa msimu huu wa 2018/19  akiwa na  kikosi chake cha Simba, ametwaa ubingwa wake wa sita Ligi Kuu Tanzania Bara.

Dar es Salaam. Unaweza kusema kiungo wa Simba, Haruna Niyonzima anabahati kutokana na mafanikio aliyoyapata tangu atue nchini kucheza soka la kulipwa.

Kiungo huyo aliyetua nchini mwaka 2011 akitokea APR ya Rwanda, alisema siri ya mafanikio yake ni uvumilivu ambao amekuwa nao pamoja na kupitia changamoto kadhaa.

 “Nimeishi vizuri Tanzania na najivunia kwakweli mafanikio ambayo nimeyapata, siwezi kusema kuwa mimi ni bora kuliko wengine ila nachoweza kusema ni mapenzi ya Mungu, nikiwa Yanga nilijitahidi kucheza kwa uwezo wangu ili kuisaidia klabu.

“Nashukuru Mungu kwa sababu nilikuwa na maisha mazuri Yanga kwa kushinda karibu kila kombe nchini,lakini kama unavyojua maisha ya mpira ni safari, nikajiunga na Simba ambako nilikuwa nikusumbilia na majeraha,” alisema.

Niyonzima alipotua nchini alijiunga na Yanga wakiwa wametoka kuchukua ubingwa wa Ligi kwa msimu wa  2010/11 hivyo ilimbidi asubiri hadi  2012/13 ambapo alibeba ubingwa wake wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara kabla ya kuchukua mfululizo kwenye miaka ya 2015,2016 na 2017.

Akiwa na kikosi cha Yanga, Niyonzima ametwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara nne, akiwa Simba hii ni awamu yake ya pili mfululizo.