Ninja presha tupu Simba

HESABU za Simba kushinda mechi mbili dhidi ya Ndanda FC na Singida United, yakienda sawa watakuwa wamefanikiwa kutetea ubingwa, lakini kwa beki wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ itakuwa maumivu makali kwani ndoto yake ya kuvaa medali itakuwa imeyeyuka.

Ninja aliliambia Mwanaspoti ndoto kubwa baada ya kusaini Yanga msimu huu wa 2018/19 ilikuwa ni kuvaa medali za kwenda kucheza kimataifa, akidai kila anapopiga mahesabu kwa sasa anaona magumu, hivyo anabakia kuwaombea Simba wapoteze mechi zao ili wao wachukue nafasi.

Simba wakiwafunga Ndanda FC kisha Singida United, watakuwa na jumla ya pointi 91, Yanga wao wakimaliza michezo yao miwili kwa ushindi watakuwa na pointi 89, hesabu hizo ndizo zinazomchanganya Ninja na akifikiria watani wao Wanamsimbazi wana michezo minne.

“Ni kweli Simba imebakiza mechi nne, mfano wakipoteza mchezo mmoja na kutoka sare michezo mitatu watakuwa na pointi 88 sisi tukishinda zote tutakuwa na 89, yote yanawezekana kwani huu ni mpira na sio maneno.

“Kiukweli kabisa kama kuna kitu nilikuwa nakitamani sana baada ya kusaini Yanga ni kuvaa medali na ndio maana tulivyotolewa FA ambako tulionekana kuwa na nafasi kubwa, nililia kwa uchungu kuona ndoto yangu inaweza isitimie,” alisema

Ninja alisema shauku hiyo ni kutokana na tangu asajiliwe Yanga hajawahi kubeba ubingwa hivyo alitarajia msimu huu ndoto hiyo ingetimia huku akisisitiza kwake ni tofauti na wengine ambao walishazivaa medali hizo.

Wakati Ninja akiweka wazi hisia zake za kutamani medali, winga wa timu hiyo Deus Kaseke alisema ulikuwa msimu wa aina yake kwao akidai walipambana walivyoweza ingawa kwa sasa anaacha hesabu ziamue.

“Hakuna mchezaji asiyependa ubingwa kwani ndio kifuta jasho kwa kazi ya msimu mzima, tulipofika kwa sasa hatuna budi kuacha hesabu ya soka ichukue nafasi yake kwani hakuna kingine cha kufanya, ngoja tuone mpaka dakika ya mwisho,” alisema.