Ninja anapofungua ukurasa mpya nchini Marekani

Muktasari:

Majeraha na kushuka viwango kwa baadhi ya wachezaji wa Yanga wanaocheza nafasi ya ulinzi kumlipa Ninja nafasi ya kuwa mchezaji muhimu hasa katika mechi za mzunguko wa pili za msimu uliomalizika 2018/2019.

Dar es Salaam.Mwaka 2019 unaweza kuwa wenye historia ya kipekee kwa beki Abdallah Shaibu ‘Ninja’.

Ni mwaka ambao ulipandisha chati jina la Ninja katika medani ya soka ndani ya muda mfupi, lakini pia ulikaribia kumporomosha beki huyo na mwisho wa siku umekuwa wa neema kwake.

Baada ya msimu wake wa kwanza ndani ya Yanga 2017/2018 kuwa mgumu akiicheza kwa mara ya kwanza akitokea Taifa Jang’ombe ya Zanzibar. Mwaka 2019 ulianza kuwa wa faraja kwa Ninja baada ya kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha Yanga.

Majeraha na kushuka viwango kwa baadhi ya wachezaji wa Yanga wanaocheza nafasi ya ulinzi kumlipa Ninja nafasi ya kuwa mchezaji muhimu hasa katika mechi za mzunguko wa pili za msimu uliomalizika 2018/2019.

Haikushangaza Ninja akitajwa kama mmoja wa mabeki waliofanya vizuri katika msimu uliomalizika huku kundi kubwa la wadau wa soka likiamini anastahili kuwemo katika kikosi bora cha msimu.

Nyakati ngumu

Hata hivyo pamoja na kufanya vyema katika msimu uliomalizika, Ninja alijikuta akipita katika kipindi kigumu ambacho kingeweza kumuathiri kisaikolojia na kuwa chanzo cha anguko lake.

Mipango ya Yanga kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao, ilimuweka Ninja katika sintofahamu kwa kutokuwa na uhakika kama ataongezewa mkataba au ataondoka.

Yanga inadaiwa ilikuwa kimya pasipo kumjulisha chochote beki huyo huku tetesi zikidai kuwa haikuwa katika mipango ya kuendelea naye.

Neema

Hata hivyo katika hali ya kushangaza, dakika za jioni, Yanga baada ya kukamilisha usajili wa wachezaji wapya na kuwaongeza mikataba wale wa zamani, ilifufua mpango wa kumbakiza Ninja lakini ilikuwa kama imechelewa.

Muda ambao walionyesha nia ya kuendelea kubaki naye, tayari alishakuwa amechukua uamuzi wa kuachana na klabu hiyo na kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi. Ninja tayari alikuwa amepata ofa ya kujiunga na MFK Vyskov inayoshiriki Ligi Daraja la Tatu nchini Czech

“Nilikuwa na malengo ya kufika mbali na ndio maana sikutaka kuikubali ofa ya Yanga ambayo walinipa baada ya kumaliza mkataba wao wa miaka miwili, nahitaji kupata changamoto mpya,” alisema Ninja.

Atua Marekani kibabe

Hata hivyo baada ya kusaini mkataba huo wa miaka minne, Ninja amekutana na bahati ya kipekee ya kupelekwa kwa mkopo kwenye klabu ya LA Galaxy inayoshiriki Ligi Kuu ya Marekani.

“Ni kweli nitaenda Marekani kucheza kwa mkopo kwenye klabu ya LA Galaxy.

“Kwangu mimi hili ni jambo kubwa na naamini ni nafasi yangu ya kupiga hatua kubwa kisoka. Kwa sasa nipo kwenye maandalizi kwa ajili ya kukamilisha safari ya kwenda huko,” anasema Ninja.

Changamoto

Ninja anafichua kuwa hana wasiwasi wa kucheza soka la kulipwa  Marekani na yuko tayari kukabiliana na changamoto mpya.

“Najua changamoto kubwa ni suala la lugha lakini hainipi shida kwa sababu lugha ya soka inafahamika na kama mnavyoona kuna wachezaji wa kigeni hapa nchini hawafahamu Kiswahili, lakini baadaye wanamudu. Kwangu naamini jambo la msingi ni kujitahidi na kuonyesha kiwango bora ingawa pia nimejipanga kujifunza Kiingereza.

Lakini kingine ni kuwa na nidhamu na kufuata kile ambacho benchi la ufundi litakuwa linaniagiza nifanye,” anasema Ninja ambaye alibatizwa jina hilo akifananishwa na beki hodari wa zamani wa Yanga, Salum Kabunda ‘Ninja’.