Ninja ainyima Simba ubingwa

BEKI wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ameutazama ushindani ulioonyeshwa katika mechi tano za Ligi Kuu Bara, kisha akatamka kuwa taji la msimu huu ni la jasho kwa timu itakayofanikiwa kulichukua.

Ninja alisema nje ya Simba na Yanga anaiona Azam jinsi ilivyo ya moto na kwamba, kama itakosakosa ubingwa basi haiwezi kuwa chini ya nafasi ya pili, endapo tu ikiendelea na kiwango ilichoanza nacho kinachowafanya wakae kileleni kwenye msimamo wa ligi.

Azam ndio timu pekee iliyoshinda mechi zote tano zinazowafanya waongoze ligi wakiwa na pointi 15, jambo ambalo Ninja analiona linatoa taswira ya jinsi ambavyo Simba na Yanga zinavyotakiwa kujituma zaidi.

“Ushindani uliopo hasa wa kuwania taji la ligi sio kwa Yanga na Simba pekee, bali hata Azam imo ndani na kama ikikosa ubingwa basi itamaliza mshindi wa pili, kikosi chao ni moto,”alisema.

“Ushindani huo unaleta ubora wa soka letu, kujua hakuna kitu cha lelemama kupata matokeo, kwa maana ya kila mchezaji kupigania timu yake ili kuweza kufanya vyema.”

Mbali na hilo, Ninja alisema bado anaamini nafasi yake ipo Taifa Stars ila ni suala la muda, na ukifika basi atalitumikia taifa.

“Sina wasiwasi na hilo, kila kitu kina muda wake ukifika basi kila kitu kitakaa mahala pake,” alisema.