Ninja:Yanga ikitumia vyema dirisha dogo ni bingwa

Muktasari:

Beki wa zamani wa Yanga, Abdallah Shaibu 'Ninja' amesema usajili uliofanywa na timu hiyo msimu ulioisha uwe funzo kupata wachezaji bora dirisha dogo.

BEKI wa zamani wa Yanga, Abdallah Shaibu 'Ninja' ameishauri timu hiyo kusajili maeneo muhimu yatakayowasaidia kutwaa taji la ubingwa kwa msimu huu baada ya kuukosa mara mbili mfululizo.
Ninja anayekipiga LA Galaxy ya Marekani, amesema kuna haja Yanga kufanya umakini wa kufuatilia wachezaji ambao watakuwa na majibu ya kuleta ubingwa na sio kukurupuka kusajili ili mladi.
"Kuna maeneo muhimu ambayo Yanga inatakiwa isajili, mfano wapate mshambuliaji wa kuamua matokeo kwenye mechi ngumu mfano kama alivyo Meddie Kagere wa Simba, akiwepo pale mbele mabeki wanahaha,"
"Msimu uliopita unaweza kuwa funzo kwao kama walisajili wachezaji wengi wanapaswa kupima kama walikuwa na msaada au la, wakijua hilo wataanzia hapo kuponya tatizo,"amesema.
Amesema anaamini Yanga ikitumia vyema dirisha dogo la usajili basi inaweza ikatwaa ubingwa ambao mashabiki wana hamu kuupata baada ya kukosa kwa miaka miwili mfululizo.
"Raha wa mashabiki wa Simba na Yanga nikuona timu zao zinachukua ubingwa, inapotokea wanaukosa basi hali inakuwa mbaya kwao,"amesema.