Nigeria, Cameroon hatari tupu AFCON hao Brazil

Muktasari:

  • Fainali za michuano ya AFCON kwa vijana inaendelea jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Taifa na Chamazi.
  • Washindi wanne watakaokwenda hatua ya nusu fainali, watakuwa wamekata tiketi moja kwa moja ya kwenda Brazil kucheza Kombe la Dunia kwa wachezaji wenye umri huo.

Dar es Salaam. Ni timu mbili tu kutoka makundi yote mawili A na B katika mashindano ya AFCON kwa vijana chini ya miaka 17, zimefanikiwa kufuzu kwa nusu fainali na kukata tiketi ya kucheza Kombe la Dunia Brazil.

Timu hizo kati ya nane kutoka Kundi A ni Nigeria na B ni Cameroon, sita zikisubiri mechi zao za mwisho za kukamilisha michezo ya hatua za makundi.

Kundi A, mbali na Nigeria kufuzu baada ya kushinda mechi zao mbili walipoifunga Serengeti Boys na Angola na sasa inajipanga kwa mchezo wa mwisho ambao watamaliza na Uganda.

Timu inayofanya katika kundi hilo ni Uganda ambao wana pointi tatu ambazo ni sawa na Angola wakitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa na Serengeti Boys haina pointi ikiwa mkiani mwa kundi.

Nafasi ya Serengeti Boys katika kundi hilo ni finyu kufuzu hatua ya nusu fainali, kwani inavizia ushindi wa mchezo wao wa mwisho na Angola. Lakini ikifikisha pointi tatu na Uganda akaifunga Nigeria ndiyo itakuwa timu ya pili kufuzu kwa sababu itakuwa na pointi sita.

Pia, hata kama watakuwa na pointi hizo tatu na Uganda akafungwa, kitakachofanyika hapo ni mahesabu kwani zote zitakuwa na idadi sawa ya pointi na kitakachoangaliwa ni mabao ya kufunga na kufungwa.

Upande wa Kundi B, Cameroon ndiyo wamefuzu, Senegal ina pointi tatu ambazo ni sawa na Guinea huku Morocco ikiwa na moja. Michezo hiyo ya mwisho ndio itatoa mshindi wa pili.

Cameroon atacheza na Senegal wakati Guinea atakipiga na Morocco.  Senegal ndio yenye nafasi kubwa kwani wakishinda mchezo huo watakuwa na sita lakini wakifungwa na Guinea au Morocco moja wapo ikishinda ndio itaenda. Pia, matokeo ya sare kwa Morocco na Guinea yataibeba Guinea nusu fainali.