Ni vita ya vigogo FDL kurudi VPL

Muktasari:

Timu nne za chini katika kila kundi zitashuka daraja moja kwa moja

Dar es Salaam. Ligi Daraja Kwanza (FDL) inaanza kutimua vumbi leo kwa michezo miwili kuchezwa katika kusaka nafasi ya kupanda Ligi Kuu msimu ujao.

Jumla ya timu 20 zinawania nafasi mbili za kupanda moja kwa moja Ligi Kuu, wakati nne zikiingia katika ‘play off’ kuwania nafasi mbili nyinghine kutimiza timu nne mpya Ligi Kuu msimu ujao. Jumla ya timu nane zitashuka daraja moja kwa moja.

Timu hizo zimewekwa katika makundi mawili, Kundi A lina timu za Ndanda FC, African Lyon, African Sports, Boma, Gipco, Lipuli, Mawenzi, Majimaji, Mbeya Kwanza na Njombe Mji.

Zilizoko Kundi B ni Alliance, Mbao FC, Singida United, AFC, Fountain Gate, Kitayosce, Geita Gold, Pamba FC, Rhino Rangers na Transit Camp.

Ni timu sita pekee ambazo hazikuwahi kuonya ladha ya Ligi Kuu, ambazo ni Boma, Kitayosce, Fountain Gate, Geita Gold, Gipco na Mawenzi, ambazo zitakuwa na kazi mbele ya vigogo wengine.

Hilo linawafanya vigogo hao wa zamani wa Ligi Kuu Tanzania Bara kuwa na wakati mgumu kwa vijana wapya, ambao wana uchu wa kupanda daraja kutokana na kushuka kwa timu nane katika makundi yote.

Uwanja wa Uhuru, African Lyon itaikaribisha Ndanda FC iliyoshuka daraja msimu huu na sasa inatupa karata yake ya kwanza kwenye Kundi A.

Mchezo mwingine utakuwa wa Kundi B, wakati wageni wa FDL, Fountain Gate ikiikaribisha Alliance iliyoshuka daraja katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Shughuli kubwa ya michezo hiyo ni kuziona timu zilizoshuka daraja kutaka kurudisha heshima yao kwa kupata ushindi kwenye michezo ya leo.

Kocha wa Alliance FC, Daddy Gilbert alisema anajivunia kuwa na vijana wenye damu changa na anaamini watafanya makubwa kwenye ligi na kurudi Ligi Kuu.

“Hatuna hofu maana tumejiandaa vizuri, tunacheza na kuwapa heshima wapinzani wetu kwa kuwa kila timu ina mipango yake, tunachoweza kusema watu wa Dodoma watarajie kupata burudani.

“FDL ni ligi ngumu na muhimu kwa upande wa maendeleo ya soka maana huku ndiko wanakotoa wachezaji wa timu ya taifa, na hii ni moja ya ligi ngumu na mchezaji anayeonyesha uwezo hapo ndipo sehemu ya kutoka,” alisema Gilbert.

Kocha wa Fountain Gate, Mohamed Muya alisema wamekamilisha maandalizi yao na timu ipo vizuri kwa kuwakabili wapinzani na ana matumaini watavuna alama katika mchezo wa leo.

“Huu ni msimu wetu wa kwanza kwenye ligi, lakini ndani tuna wachezaji wenye uzoefu ambao watasaidiana na vijana wetu na kuifanya timu kuwa bora zaidi,” alisema Muya.

Ligi hiyo itaendelea kesho kwa michezo miwili ya Kundi A, Njombe Mji ikiikaribisha Mbeya Kwanza kwenye Uwanja wa Sabasaba, African Sports ikicheza na Majimaji kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Mbeya Kwanza tayari imefanya mabadiliko ya benchi lake la ufundi na sasa inaongozwa na Stephen Mtata, ambaye anarekodi tamu ya kufundisha timu kadhaa za Daraja la Kwanza, huku Michael Mnyali akiwa kocha msaidizi.

Kwenye Kundi B, Kitayosce inayonolewa na Idd Cheche itaikaribisha Transit Camp kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora na Geita Gold ikicheza na Singida United.

Kocha wa Transit Camp, Emmanuel Gift amejigamba kuwa na timu imara, ambayo msimu ujao watakuwa ni miongoni mwa timu zitakazopanda Ligi Kuu.

Msimu uliopita, Transit Camp ilitinga hadi hatua ya mtoano na kutolewa kwa matuta na Ihefu SC baada ya sare ya mabao 3-3 kwenye michezo miwili.

Msimu uliopita zilishiriki timu 24 lakini kutokana na mabadiliko ya kanuni zimepungua na kuwa 20, msimu ujao zitapungua tena timu na kufikia 16.

Timu zitakazoongoza kila kundi zitajihakikishia kupanda Ligi Kuu moja kwa moja, zitakazomaliza nafasi ya pili na tatu zitacheza hatua ya mtoano ili kubaki.