Ni vita ya usajili dirisha dogo Ligi Kuu

Muktasari:

Chirwa raia wa Zambia, amemwaga wino Azam baada ya kuvunja mkataba na Klabu ya Nogoom FC ya Misri kwa madai ya kushindwa kumlipa mshahara na posho.

Dar/Mwanza. Wakati pazia la usajili kwa klabu zinazoshiriki Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza limefunguliwa rasmi, Azam FC imekuwa ya kwanza kumsajili mshambuliaji Obrey Chirwa.

Mchezaji huyo anakwenda Azam kutengeneza pacha na Donald Ngoma, aliyewahi kucheza naye pamoja wakiwa kwa mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu, Yanga.

Chirwa raia wa Zambia, amemwaga wino Azam baada ya kuvunja mkataba na Klabu ya Nogoom FC ya Misri kwa madai ya kushindwa kumlipa mshahara na posho.

Wimbi la wachezaji wa ndani wanaotaka kuzihama klabu zao kwa sababu tofauti ikiwemo kukosa nafasi za kucheza, linatarajia kufuata nyayo za Chirwa katika usajili wa dirisha dogo lililofunguliwa jana kabla ya kufungwa Desemba 15.

Usajili wa msimu huu unaweza kutikisa kutokana na idadi kubwa ya wachezaji waliong’ara msimu uliopita kutaka kuzihama klabu zao mpya baada ya kukosa nafasi ya kuendeleza makali yao ya awali.

Washambuliaji watatu wa Simba, Mohammed Rashid, Marcel Kaheza na Adam Salamba, wanapewa nafasi ya kuondoka kwa mkopo baada ya kukosa nafasi ya kucheza.

Itakumbukwa Rashid alikuwa mfungaji bora wa Prisons kama ilivyokuwa kwa Kaheza (Majimaji) na Salamba aliyewika Lipuli, walitikisa vyombo vya habari kutokana na ubora wao wa kufunga mabao.

Rashid anahusishwa kurejea Prisons, Salamba (bado haijajulikana), Kaheza (KMC) na kipa anayesugua benchi Said Mohammed amewekwa sokoni kwa mkopo.

Mchezaji mwingine Wazir Junior aliyetesa katika kikosi cha Toto Africans msimu uliopita kabla ya kutua Azam anakosugua benchi anatajwa kujiunga na Biashara United.

Prisons imetuma maombi ya kuwasajili mchezaji wa Yanga, Emmanuel Martin, Ditram Nchimbi aliyeng’ara msimu uliopita akiwa na Njombe Mji kabla ya kutua Azam. Mwingine ni Eliuter Mpepo aliyetimka Singida United.

Coastal Union imeanza mchakato wa kumrejesha kinda wake wa zamani, Juma Mahadhi, aliyewika katika kikosi hicho kabla ya kujiunga na Yanga anakosugua benchi.

Mchezaji mwingine anayeweza kutikisa usajili huo ni kinda, Yusuph Mhilu wa Yanga ambaye anawindwa na Polisi Dar es Salaam inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.

Beki wa kushoto wa Yanga, Haji Mwinyi amepokwa namba na Gadiel Michael, lakini ubora wake umeivutia AFC Leopards ya Kenya inayomtaka.

Akizungumza jana, Kocha wa Azam Hans van der Pluijm, alisema hana uhakika kama ataingia sokoni kusaka nyota wapya, lakini tayari ameshawatupia jicho baadhi ya wachezaji.

Kocha wa KMC, Etienne Ndayiragije alisema ana tatizo la safu ya ushambuliaji na tayari amemsajili nyota wa zamani wa Simba, Elias Maguli.

“Maguli ni mchezaji mzuri ambaye tunaamini anaweza kutusaidia kutokana na uzoefu alionao. Tuna mpango wa kuongeza kiungo ili kuongeza nguvu kwenye eneo hilo,” alisema Ndayiragije ambaye misimu miwili iliyopita ya Ligi Kuu alikuwa akiinoa Mbao FC ya Mwanza.

Kocha wa Ruvu Shooting, Abdulmutik Haji ‘Kiduu’ alisema katika dirisha dogo anataka kuwaongeza washambuliaji ili kuimarisha kikosi chake.

Kwa upande wake, Kocha Ally Bizimungu wa Mwadui Shinyanga, alisema atasajili kiungo na mshambuliaji. Amri Said wa Mbao, alisema ataongeza kipa, beki wa kulia, kushoto, kati, kiungo na mshambuliaji wa pembeni. Kocha wa Biashara United, Thierry Hitimana, alisema atawasajili washambuliaji wawili wenye uwezo wa kufunga mabao.

Imeandaliwa na Eliya Solomoni, Thomas N’gitu, Saddam Sadick