Ni muda wa mafahari watatu Mond, Kiba, Konde Boys kutoa songi la pamoja

Muktasari:

Sisi ni dunia. Sisi ni watoto. Sisi ndio ambao tutaifanya siku ing’are, hivyo hebu tutoeni. Kuna chaguo ambalo tunalifanya. Tunaokoa maisha yetu wenyewe. Ni kweli tutaitengeneza siku iliyo bora, ni wewe na mimi.

UNAWADIA wakati. Tunapopaswa kuzingatia wito fulani. Pale dunia lazima ijikusanye pamoja kama kitu kimoja. Kuna watu wanakufa. Ooh, ni muda wa kunyoosheana mkono wa maisha. Zawadi kubwa kupita zote.

Hatuwezi kuendelea. Tukijiongopea siku baada ya siku. Kwamba kuna mtu, mahali fulani punde ataleta mabadiliko. Sisi wote ni sehemu ya familia kubwa ya Mungu. Na kiukweli, unafahamu, upendo ndio kila kitu tunachohitaji.

Sisi ni dunia. Sisi ni watoto. Sisi ndio ambao tutaifanya siku ing’are, hivyo hebu tutoeni. Kuna chaguo ambalo tunalifanya. Tunaokoa maisha yetu wenyewe. Ni kweli tutaitengeneza siku iliyo bora, ni wewe na mimi.

Oh, watumie moyo wako. Hivyo watajua kwamba kuna mtu anajali. Na maisha yao yatakuwa imara na huru. Kama ambavyo Mungu ametuonesha kwa kugeuza mawe kuwa mkate. Na kwa hivyo sisi wote lazima tunyooshe mkono wa kusaidia.

Sisi ni dunia. Sisi ni watoto. Sisi ndio ambao tutaifanya siku ing’are, hivyo hebu tutoeni. Kuna chaguo ambalo tunalifanya. Tunaokoa maisha yetu wenyewe. Ni kweli tutaitengeneza siku iliyo bora, ni wewe na mimi.

Unapokuwa na huzuni na umevurugwa, inaonekana hakuna matumaini kabisa. Lakini kama unaamini hakuna namna tunaweza kuanguka. Vizuri, vizuri, hebu wote tutambue. Oh, kwamba mabadiliko yanaweza kuja tu. Pale tukisimama pamoja kama kitu kimoja.

Sisi ni dunia. Sisi ni watoto. Sisi ndio ambao tutaifanya siku ing’are, hivyo hebu tutoeni. Kuna chaguo ambalo tunalifanya. Tunaokoa maisha yetu wenyewe. Ni kweli tutaitengeneza siku iliyo bora, ni wewe na mimi.

Ni shairi la wimbo “We Are The World”. Miaka 35 iliyopita, mwanamuziki ambaye pia ni staa wa filamu, Harry Belafonte, aliibuka na wazo la kujumuisha wanamuziki wakubwa Marekani kwenye wimbo mmoja ili usaidie baa la njaa lililokuwa likiikabili Ethiopia.

Belafonte alimgusa Ken Kragen ambaye alikuwa meneja wa masupastaa Lionel Richie na Kenny Rogers. Kragen alipolielewa wazo la Belafonte, aliwajulisha Richie na Rogers. Nani prodyuza? Richie akasema maneno machache na fundi wa mafundi, Quincy Jones.

Jones akasema ngoma haitabamba bila dogolee, Michael Jackson ‘MJ’, ambaye ndiye alikuwa top-artist Marekani na duniani kote. Albamu yake ya “Thriller” ilikuwa sokoni ikiendelea kuvunja kila rekodi. Kolabo la mastaa wa Marekani lingeonekana jepesi bila MJ.

Naye MJ alipoambiwa kuhusu kushiriki wimbo wa pamoja kwa ajili ya kusaidia Afrika, akamuuliza Jones: “Nani anaandika?” Jones akamtaja Richie. MJ akamwambia Jones: “Sio tu nitashiriki kuimba, bali pia nitashiriki kuuandika huo wimbo wenyewe.”

MJ akamvutia waya Richie, akamwambia: “Big Bro, hiyo ngoma huandiki peke yako. As long as ni ngoma ya kusaidia Afrika, lazima mkono wangu uhusike.” Richie angemgomeaje MJ? Mtu bee zikaketi, Richie na MJ. Ndio zikatunga hilo shairi.

Aliyekuwa mke wa Richie, Brenda Harvey, akampigia simu music mogul, Stevie Wonder, akamwambia: “Shem lake unapitwa!” Wonder akamwambia Richie: “Tusifanyiane hivyo mjomba!” Nguvu ikaongezeka.

Kragen na Belafonte walifanya kazi ya uratibu, halafu The Musical Professor, Kragen, alitimiza ufundi wake wa kuchagua nani aingie kwenye wimbo, kisha akae eneo lipi na kwa sauti gani. Hivyo ndivyo “We Are The World” ilivyoletwa mzigoni na kuibuka kuwa ngoma ya kila taifa. Huvunji sheria kama ukiita ni ngoma ya Umoja wa Mataifa.

Basi, ikawezekana kwa vichwa 22 kupeana nafasi ya kuimba. Kuanzia Richie aliyefungua dimba na ile sauti yake iliyosanifiwa kooni kwa mayai ya kware, kisha Wonder, halafu Paul Simon, akafuata Kenny Rogers, James Ingram akapokea, Tina Turner akaingia, Billy Joel akafunga verse ya kwanza.

MJ anakuja kutuimbia chorus pamoja na Dianna Ross. Ubeti wa pili unaanzishwa na madam masauti, Dionne Warwick. Willie Nelson anapokea. Al Jarreau anafanya yake, halafu Bruce Springsteen, Kenny Loggins, Steve Perry na Daryl Hall wanaimba kiitikio kwa jeuri ya misauti yao. MJ anarudi tena kuimba bridge kwa kupokezana na Huey Lewis, Cyndi Lauper na Kim Carnes, halafu kiitikio kinaimbwa pamoja na wanamuziki wote. Katika wimbo huo, Bob Dylan na Ray Charles, walifanya yao katika upper notes, wakati MJ, Wonder na Springsteen waliingiza harmony vocals kibingwa.

Ni kazi yenye umri wa miaka 35 sasa, walioimba wengi wao ni mababu na mabibi, wachache walishatangulia mbele za haki. Baa la njaa Ethiopia, likalazimisha wa watu kutunga wimbo wa hisani. Kisha ikazaliwa albamu yenye jina “We Are The World”. Nakala 20 milioni ziliuzwa. Fedha dola 63 milioni, zilipatikana kwenye mauzo na zikaepelekwa kuokoa Waafrika waliokuwa wakifa njaa Ethiopia. Watu zaidi ya milioni moja walifariki dunia Ethiopia kati ya mwaka 1983 na 1985. Mradi huo uliitwa “US for Africa”. Wacanada walichangia wimbo kwenye albamu hiyo, unaitwa “Tears Are Not Enough”. Ndio, machozi peke yake hayatoshi.

Wacanada walijiita The Northern Light. Wanaimba kutaka daraja lijengwe kati ya watu wa dunia ili wenye uhitaji wasaidiwe. Haitoshi kutoa machozi, bali kufungua moyo na kuwasaidia wenye matatizo.

Ni mzuka ambao nimekuwa nao kusikiliza nyimbo za hisani, kipindi hiki dunia inateswa na janga la maradhi ya Covid-19, yanayosababishwa na virusi vya SARS Corona2. Nyimbo za kukumbushana kujali ni muhimu sana.

Covid-19 inaua maelfu Italy. Imeshatua Marekani na maambukizi ni ya haraka kuwahi kutokea. Hispania ni janga hasa. China wamefanikiwa lakini maelfu wameshapoteza maisha. Afrika imeshavamiwa.

Covid-19 ipo Tanzania. Yupo wapi Belafonte wa Bongo aanzishe wazo ili tuimbe “Sisi ni Watanzania. Familia ya Nyerere”. Huu ndio wakati wa Diamond Platnumz, Ali Kiba, Harmonize na mastaa wengine kuimba pamoja wimbo wa hisani kwa ajili kukuza uelewa wa watu kuhusu Covid-19 na kuchangisha fedha kwa watakaokuwa wanapitia mazingira magumu zaidi.

Usikike wimbo wenye upendo na unaopalilia urafiki wa shida na raha kama “That’s What Friends Are For” Dionne Warwick, Elton John, Stevie Wonder na Gladys Knight walivyoimba kwa fahari kubwa ya utajiri wa sauti zao.

Mama la mama Dionne anatimiza wajibu vyema kama mmiliki wa wimbo, Elton kachezea piano na sauti yake dhahabu, Wonder anapuliza harmonica, halafu anapanda na kushuka kwa sauti yake iliyomjaza utajiri, kisha mshindi wa wakati wote linapokuja shindano la sauti za juu, Gladys Knight, ni kazi bora iliyowezesha kupatikana dola milioni tatu mwaka 1985 kwa ajili ya waathirika wa Ukimwi Afrika.