Ni muda muafaka sasa RT, wadau kuamka ili kuinua riadha

Muktasari:

  • Sio mbio hizo tu, hatakatika mbio kama Rock Marathon, Kilimanjaro Marathon, sijui KIA na nyinginezo kubwa hapa nchini zimekuwa zikitawaliwa kwa muda mrefu na wanariadha kutoka nje ya nchi hususani Wakenya, kuonyesha kuwa Tanzania kwa sasa imeachwa mbali katika mchezo huo.

MIAKA ya 1970 hadi 1990 Tanzania ilikuwa ikitamba kwenye mchezo wa riadha na hasa mbio ndefu. Katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati haikuwa ikishikika na ndio maana haikuwa ajabu katika miaka hiyo kushuhudia wanariadha wetu wakitwaa medali mbalimbali.

Wanariadha kama Filbert Bayi, Juma Ikangaa, Andrew Sambu, Suleiman Nyambui, Restituta Joseph na wengine walitetemesha kwenye mchezo huo mbele ya wanariadha wa mataifa mengine. Katika miaka hiyo wanariadha wa Tanzania ndio waliokuwa wakitetemesha dunia kwa Mataifa ya Afrika kwa sababu ya mafanikio yao.

Kenya, Ethiopia ambazo leo zimekuwa watawala kwenye mchezo huo kwa sasa hazikuwa zikifua damu kwa Tanzania. Hata hivyo sijui umepita upepo gani, leo Tanzania imekuwa ikiburuzwa na Wakenya sambamba wa Ethiopia na hata Eritrea ambao hawakuwahi kutikisa kabla ya hapo.

Leo sio ajabu kusikia wanariadha wa Kenya wakija kutawala kwenye mbio za kimataifa zinazofanyika nchini, mfano mdogo Jumamosi iliyopita Wakenya walikuja na kuwatambia Watanzania kwenye mbio za Ngorongoro nus Marathoni.

Sio mbio hizo tu, hatakatika mbio kama Rock Marathon, Kilimanjaro Marathon, sijui KIA na nyinginezo kubwa hapa nchini zimekuwa zikitawaliwa kwa muda mrefu na wanariadha kutoka nje ya nchi hususani Wakenya, kuonyesha kuwa Tanzania kwa sasa imeachwa mbali katika mchezo huo.

Hii ni tofauti na ilivyokuwa enzi hizo, ukisikia zinafanyika mbio za Mount Meru Marathon, basi washindi ni lazima wawe Watanzania kuanza nafasi zote za juu, lichja ya kuwepo kwa wanariadha kibao wa mataifa mengine ya kigeni.

Nini kilichotokea kwenye mchezo huo nchini? Tanzania imekosea wapi ama imejikwaa wapi na ifanye nini kujikwamua? Haya ni maswali ambayo wadau wa riadha wanapaswa kujiuliza. Ndivyo ambavyo mabosi wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) wanapaswa kujiuliza na kutafuta majibu kwa haraka.

Kuna sehemu Tanzania imekosea na lazima irekebishe, ili kurejesha heshima ya wanariadha wa Tanzania kwenye anga za kimataifa. Mwanaspoti kama wadau wa michezo, tunaamini bado tuna nafasi ya kusahihisha makosa baada ya kujitathmini kisha kuanza upya kurejesha heshima ya mchezo huo kwa Tanzania.

Tunaamini Tanzania inaendelea kuzalisha vipaji vya mchezo huo riadham, ila ni kwamba kwa kuwa hakuna mipango mizuri ya kuvikuza na kuviendeleza kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, ndio maana tunashindwa kunufaika nao.

Serikali, RT na wadau wa mchezo huo ni lazima wakae chini kwa sasa na kuangalia namna ya kurudi kwenye mstari ili kuiepushia aibu nchi ya kuburuzwa kwenye riadha na mataifa ambayo yalikuwa nyuma miaka kadhaa nyuma kabla ya kubadilisha kibao.

Bado muda upo, vipaji vipo na wanariadha wapo ili kuibeba nchi, muhimu ni kuwepo kwa mpango mkakati wa kuhakikisha riadha inarudi kwenye mstari mnyoofu na kuanza kurejesha heshima.

Inawezekana, kukosekana kwa mipango mizuri na miundo mbinu ya kuwapa nafasi vijana wenye vipaji katika riadha kuukacha mchezo huo na kukimbilia kwenye michezo mingine kwa kuona inapewa kipaumbele na ina miundo mbinu myepesi, hata kama nako bado kama nchi tunachechemea.

Riadha ni mchezo wenye utajiri mkubwa ambao leo umewatajirisha wanariadha wa Ethiopia, Kenya na kwingineko duniani na kama Tanzania ingetambua fursa hiyo ingeweza kukomaa kuwatengenezea mazingira mazuri vijana wetu kujitajirisha kupitia mchezo huo.

Miji ambayo ilikuwa ikisifika kwa kuzalisha wanariadha nyota kama ya Manyara, Arusha, Singida, Kondoa na kwingineko bado ipo na bila shaka vijana wenye vipaji wanaendeleza kuzaliwa, ni wakati ya kufuatiliwa na kuwekewa mikakati ya kuwaendeleza ili waje walinufaishe taifa na wenyewe.

Kupitia mashindano ya michezo shuleni inaweza kusaidia kuwaibua na kuwaendeleza vijana wenye vipaji vya riadha na kuwepo kwa mkakati maalum kama uliopo kwenye soka ambao umekuwa wakati mwingine ukisaidia kuwaendeleza wanasoka chipukizi ambao wamekuja kuwa mashukaa wa taifa. Pia kuwepo kwa mashindano mbalimbali ya vijana itasaidia taifa ili kuwaibuka wanariadha wapya.