Ni moto wameibeba Simba nje ndani

Muktasari:

  • Makala haya inakuletea baadhi ya watu ambao wapo ndani ya Simba kwa namna moja au nyingine kuifikisha timu hiyo ilipo.

MSIMU huu wa Ligi ya Mabingwa Afrika Simba wameweka rekodi kuwa timu ya kwanza kutoka Tanzania kucheza robo fainali ya mashindano haya makubwa kwa ngazi ya klabu Afrika tangu yalivyo badilishwa muundo wa uendeshaji 1997.

Mafanikio makubwa ambayo waliyapata katika mashindano haya timu kutoka Tanzania ilikuwa 2003, ambapo klabu ya Simba ilifika katika hatua ya makundi na mpaka sasa inafika miaka 15, hakuna timu iliyofanya hivyo.

Makala haya inakuletea baadhi ya watu ambao wapo ndani ya Simba kwa namna moja au nyingine kuifikisha timu hiyo ilipo.

MO DEWJI

Mdhamini wa Simba; Mohammed Dewji ‘MO’ mara ya mwisho Simba inafika hatua ya makundi 2003, alikuwa katika timu hiyo lakini tangu ameondoka timu hiyo imeshindwa kufikia mafanikio hayo ambayo inapita miaka 15. Msimu huu Simba imefanya mabadiliko ya uendeshaji timu na wapo katika hatua ya mwisho timu hiyo kuendeshwa kibiashara na mwekezaji aliyeshinda zabuni ni MO ambaye amekuwa akikibeba kikosi hicho kila inapoiitwa leo.

MO ameibeba timu katika maeneo muhimu ambayo wakati hakuwa ndani ya timu viongozi waliokuwa madarakani walikuwa wanapitia wakati mgumu, maeneo hayo ni kama kulipa mishahara mizuri kwa wachezaji na wafanyakazi wote.

Wachezaji na benchi la ufundi mbali ya kupata mishahara mizuri tena kwa wakati, wanapata posho, wanaishi katika hoteli nzuri, wanasafiri bila shida na wanakwenda kuweka kambi katika maeneo ambayo watakuwa wanahitaji kwa wakati huo bila ya kizuizi chochote. Kama haitosho, MO alimwaga mkwanja katika usajili wa wachezaji wa maana ambao leo hii wanaipaisha Simba katika mashindano hayo kutokana na mchango wao wanaoutoa ndani ya timu lakini alitafuta benchi la ufundi lililokuwa na makocha wa maana.

PATRICK AUSSEMS

Wamepita makocha wengi ndani ya miaka 15, ambayo Simba walikuwa wakiona rekodi ya kucheza hatua kubwa ya makundi wakicheza timu nyingine kutoka katika Mataifa mengine na ilifikia muda mwingine hawakushiriki kwani ilipita zaidi ya miaka mitano bila kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara. Msimu huu Simba walifanya mabadiliko katika benchi la ufundi baada ya kuachana na kocha Mfaransa Pierre Lechantre na kumchukua Mbelgiji, Patrick Aussems ambaye aliingia mkataba na mabosi wa timu hiyo kuipeleka hatua ya makundi.

Aussems ambaye mwanzoni hakuwa akieleweka haswa na mashabiki wa Simba baada ya kumuacha kocha msaidizi Mrundi Masoud Djuma lakini aliweza kuitengeneza na kuwa hatari zaidi katika mechi zilizokuwa zinafuata.

Ni wazi Aussems ameitengeneza Simba kuwa timu hatari zaidi hasa inapocheza uwanja wa nyumbani na kuweza kuvuna pointi tisa ambazo zilitosha kuwapeleka katika hatua ya robo fainali ambayo wapo sasa.

DENIS KITAMBI

Awali Simba ilikwenda katika mechi nne za hatua ya makundi bila ya kuwa na kocha msaidizi huku Aussems akiwa kwenye benchi anafanya kazi mwenyewe na hilo huenda lililichangia kupoteza mechi mbili za ugenini kwa kufungwa mabao 10.

Aussems alionekana anakosa usaidizi sahihi katika benchi la ufundi la Simba kwani kulikuwa na makocha Muharami Mohammed ‘Shilton’ ambaye amebobea katika kuwanoa makipa n ahata Adel Zrane nae ni mzuri katika kutengeneza ufuti wa wachezaji.

Mechi ya kwanza Simba ilicheza kwenye benchi kukiwa na Kitambi ilikuwa dhidi ya JSS ugenini ambapo Simba walipoteza kwa kufungwa mabao 2-0, lakini walicheza vizuri kuliko mechi zote walizocheza ugenini katika mashindano hayo. Kitambi alionekana kumpa ushahuri mzuri katika mechi hiyo na JSS ambayo Simba walionekana kuwa na mabadiliko lakini kama haitoshi alilifanya hilo tena katika mechi ya mwisho na AS Vita ambayo walionekana kufanya hata mabadiliko ambayo yalikuwa na tija.

Kitambi kwa muda mfupi alikuwa Simba mpaka hivi sasa akichukua mikoba ya usaidizi kutoka kwa Djuma ameonekana kuwa na mchango sahihi katika nenchi la ufundi la timu hiyo mpaka kuweza kufuzu katika hatua ya makundi.

ADEL ZRANE

Kocha wa viungo wa Simba alikuwa akitimiza jukumu la kuwatengeneza wachezaji katika hali ya ufiti na kushindana muda wote wanapokuwa uwanjani na hilo liliweza hata kujidhihirisha katika mechi ya mwisho na AS Vita wachezaji wa timu hiyo walipambana vya kutosha.

Wachezaji wa Simba msimu huu, wanaonekana kuwa fiti na hali ya kushindana muda wote wanapokuwa mazoezini na kwenye mechi wanapopewa mazoezi magumu na yote hii ni kazi ya msaidizi wa Aussems, Zrane ambaye ni wazi amehusika katika mchango wa timu hiyo kwenda robo faainali kwa kiasi kikubwa.

NYOTA WATATU

Kikosi cha Simba kina zaidi ya wachezaji 25, ambao walipata nafasi ya kila mmoja kutoa mchango wake ili kuhakikisha timu inakwenda katika hatua za mbele zaidi kama ilipofikia wakati huu. Lakini katika wachezaji hao hutaacha kuwataja watatu ambao wameonekana kutoa mchango mkubwa kwa mabao yao ambayo yalikuwa muhimu ili Simba kufika katika hatua ya robo fainali ambayo hivi karibuni watacheza.

Meddie Kagere ndio kinara wa mabao katika kikosi hiko amefunga mabao sita ambayo yalichangia kupata pointi tatu dhidi ya JSS, Al Ahly, Nkana na Mbabane Swallows kwa maana hiyo katika orodha ya wachezaji waliofanya vizuri mpaka timu hiyo ilipofikia huwezi kuacha kutaja mchango wake.

Clatous Chama amefunga mabao muhimu kabisa ambayo yamewavusha Simba kutoka katika hatua moja kwenda nyingine ambayo kama si uzoefu na umakini ya kiungo huyu fundi wasengeweza kufika ambapo wapo wakati huu. Chama alifunga mabao muhimu katika mechi mbili na Mbabane ambayo yaliipeleka Simba katika hatua ya pili dhidi ya Nkana na alifunga bao la tatu katika mechi ya marudiano na lilikuwa dakika za mwisho na muhimu kwa timu yake kwani ndio liliwapeleka hatua ya makundi.

Katika hatua ya makundi Chama hakufunga bao lolote katika mechi tano za mwanzo na alionekana kuwa mchezaji wa kawaida kana kwamba ameshuka kiwango lakini katika mechi ya mwisho dhidi ya AS Vita hapa Dar es Salaam alifunga bao la pili dakika za jioni lililoivusha Simba robo fainali.

Simba hata kama watashindwa kwenda mbali zaidi lakini hawataacha kumpongeza Chama kutokana na mabao yake muhimu ambayo yalikuwa yanaamua hatma ya timu yake.

Nahodha John Bocco alifunga mabao matatu katika mashindano haya lakini yote nayo yalikuwa muhimu mawili katika mechi ya kwanza dhidi ya Mbabane na lingine alifunga kule Kitwe, Zambia dhidi ya Nkana, Bocco mbali ya kufunga mabao hayo lakini amekuwa na mchango mkubwa katika kikosi cha Simba kwani alionekana kushindana na kupambana muda wote ambao aliwafanya kila beki wa timu pinzani kuwa katika hatihati muda wote.

VIGOGO WAZITO

Viongozi wengi wa Simba wamefanya kazi yao ipasavyo kwa kila mmoja kuifikisha timu katika hatua hiyo ya robo fainali lakini hautaweza kuacha kutaja Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori na Mjumbe wa Bodi, Salim Abdallah ‘Try Again’.

Magori muda wote alionekana kuwa na timu ilipo na alifanya kazi kwa maelewano makubwa na kocha Aussems kwa kumpatia kila ambacho alikuwa anahitaji kwa wakati ili kuhakikisha timu inafanya vizuri na kufikia malengo. Try Again alikuwa Kaimu Rais katika uongozi wa Simba uliopita na alifanya kazi nzuri kwa kusajili wachezaji wa maana kama Kagere, Wawa na wengine.

HAJI MANARA

Ofisa habari wa Simba mbali ya viongozi wa Simba kutimiza majukumu yao lakini nae alifanya kazi yake ipasavyo haswa kuhamasisha mashabiki waliojitokeza kwa wingi katika mechi zao walizocheza Uwanja wa Taifa.

Katika mechi zote za Simba ambazo walicheza nyumbani nguvu ya mashabiki ilionekana kwani walijitokeza kwa wingi.