Ni Namungo na Kagera

WAKATI Ligi Kuu Bara ikiendelea kesho Jumatano kwa mechi nne kupigwa viwanja tofauti, huko mkoani Lindi, timu ya Namungo FC na Kagera Sugar kila upande imesisitiza lazima kieleweke katika vita ya pointi tatu.

Hata hivyo, timu hizo zinakutana ikiwa kila upande unayo kumbukumbu ya kupoteza mechi iliyopita ambapo Namungo ikiwa nyumbani ililala kwa bao 1-0 mbele ya Mwadui, huku Kagera Sugar ikifa kwa mabao 4-2 dhidi ya Azam FC.

Mchezo huo ambao utapigwa katika dimba la Majaliwa unatarajia kuwa na ushindani mkali kutokana na timu zote kutokuwa na matokeo mazuri sana, hivyo kuhitaji ushindi ili kujiweka pazuri.

Kocha Mkuu wa Namungo, Hitimana Thiery alisema: “Hata mechi iliyopita hatukucheza vibaya licha ya matokeo kutokuwa mazuri, kwa sasa tunaendelea kujiweka sawa kuhakikisha Jumatano tunashinda, istoshe vijana wangu waliokuwa majeruhi wamerudi uwanjani.”

Kwa upande wake, Nahodha wa Kagera Sugar, Erick Kyaruzi alisema kuwa, “tumetoka kupoteza mchezo, kwa hiyo makosa yaliyojitokeza benchi la ufundi limeona na wachezaji hatutaki yajirudie, tunaenda kusaka pointi tatu na kujinasua chini.”