Ni Ligi Kuu England leo

London, England. Pazia la Ligi Kuu England linafunguliwa rasmi leo kwa michezo minne kutimua vumbi.

Ratiba ya ligi hiyo maarufu duniani awali ilionyesha kuwepo kwa michezo sita katika siku ya ufunguzi, lakini sasa imebaki minne baada ya ile miwili kuahirishwa.

Chama cha Soka England (FA) kiliahirisha mchezo kati ya Burnlay na Manchester United kutokana na Mashetani Wekundu kuchelewa kumaliza msimu uliopita kwa wakati kwa kuwa na mashindano ya Ligi ya Europa.

Lakini pia FA iliahirisha mchezo kati ya Manchester City dhidi ya Aston Villa kutokana na City kuwa na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Na katika mchezo wa kwanza leo, Fulham iliyopanda tena Ligi Kuu itakuwa nyumbani kuialika Arsenal.

Kocha wa Fulham na kiungo wa zamani wa Chelsea, Scott Parker alisema mchezo huo ni muhimu kwao licha ya kuwa mgumu kutokana na aina ya timu wanayokuana nayo.

Mchezo mwingine utakaofanyika leo utakuwa ule wa Liverpool dhidi ya Leeds United katika Uwanja wa Anfield.

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu watahitaji kuonyesha ubora wa msimu uliopita kwa kuanza kwa ushindi dhidi ya timu iliyopanda daraja.

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp alisema licha timu yake kusajili mchezaji mmoja tu hadi sasa, wataingia kwa tahadhari zaidi katika mchezo wa leo.

Liverpool, ambayo ipo mbioni kumsajili Thiago Alcantara ndiyo mabingwa watetezi ambao hadi sasa wamesajili nyota mmoja kutoka Olympiakos, Kostas Tsimikas.

Katika mchezo mwingine wa leo, West Ham United itakuwa na kibarua cha nyumbani kwenye Uwanja wa London watakapoialika Newcastle United.

Mtanange mwingine utakuwa katika Uwanja wa Selhurst Park, wakati Southampton watakapokuwa wageni wa Crystal Palace, ambayo ina kawaida ya kusumbua vigogo wa ligi hiyo pendwa duniani.