Ni Dakika 180 tu za SDL kuamua wa kwenda FDL

Wachezaji wa Toto Africans wakifanya mazoezi kujiandaa na moja ya mechi zao za Ligi Daraja la Pili (SDL). PICHA|MAKTABA

Muktasari:

  • Wakizungumza kwa nyakati tofauti, makocha wa baadhi ya timu hizo, wametamba kushinda mechi hizo zilizobaki ili kutimiza malengo yao.

MWANZA.LIGI Daraja la Pili imebakiza mechi mbili sawa na dakika 180 kuamua hatma ya timu moja itakayopanda Daraja la Kwanza msimu ujao lakini kundi B vita ni kali hasa kwa timu tatu kusaka nafasi hiyo.

Hadi sasa kundi hilo linaongozwa na Kumuyange FC wenye pointi 20 sawa na Gipco, huku Area C ya mkoani Dodoma wakiwa wamekusanya alama 17 na Toto Africans wakiwa na pointi 13.

Kundi hilo kwa sasa halitakuwa na timu inayopambana kushuka daraja kwani Madini FC imeshushwa baada ya kushindwa kufika uwanjani kucheza na Milambo FC.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, makocha wa baadhi ya timu hizo, wametamba kushinda mechi hizo zilizobaki ili kutimiza malengo yao.

Kocha wa Kumuyange, Mathias Wandiba alisema akili yao ipo kwenye mchezo wa Jumamosi dhidi ya Area C, kisha kuanza maandalizi ya kucheza na Gipco ambayo ni mechi ya mwisho ya ligi hiyo.

“Nafasi tunayo, kikubwa ni kujipanga kushinda mchezo kisha mechi ya mwisho na Gipco kuhakikisha tunapanda Daraja,” alisema Wandiba.

Kwa upande wa Kocha wa Gipco, Choki Abeid alisema presha ni kubwa kwenye kikosi chake kutokana na kuhitaji ushindi katika mechi hizo ili kufikia ndoto zao.

“Presha ni kubwa kwa vijana wangu kwa sababu ya kutaka mafanikio, benchi la ufundi linapambana kuwaweka sawa ili kupata pointi sita katika mechi zilizobaki na kupanda daraja,” alisema Abeid.