Ngumi zimemfanya vibaya, msoto wake hatari

Muktasari:

  • Cheka anasema, kabla mipango ya Kimbau kumchukua haijakaa sawa, kuna jirani yao mmoja alimuonea huruma namna alivyokuwa na umri mdogo, lakini anapambana kimaisha.

AKIWA na miaka 17, Bondia Francis Cheka alitoka Dar es Salaam kkwenda Morogoro bila kufahamu aatafikia wapi, lakini ndivyo akili yake ilivyomtuma kupanda basi kuelekea mji kasoro bahari.

“Mfukoni nilikuwa na Sh 20,000 pekee ambayo nilipewa na Kimbau (Shomari), ambaye ni promota wa ngumi za kulipwa,” anasimulia Cheka.

WALIPOKUTANA NA KIMBAU

Cheka anasema walikutana na Kimbau wakati huo akiwa kwenye Timu ya Ngumi ya Ngome mwaka 1999.

“Nilianza kujifunza ngumi nikiwa shule ya msingi, nilijaribu mchezo huo baada ya maisha ya nyumbani kwetu kuwa magumu. Hali ilikuwa mbaya.

“Baba yangu alikuwa mlinzi, wakati huo alikuwa ametengana na mama, hivyo mzee akawa ameoa mke mwingine, maisha ya nyumbani yalikuwa magumu sana.

“Kuna wakati hata kula ilikuwa tabu, unakwenda shule hujui ukitoka unakula nini, sikuwa na mawasiliano na mama yangu mzazi, hivyo nikaona bora niache shule nijichanganye mtaani.

“Ndipo nikaibukia kwenye Timu ya Ngome ambayo nilikwenda kufanya nayo mazoezi, kocha wao akanipenda na kunichukua moja kwa moja kwenye klabu hiyo,” anasema.

Anasema alikwenda na timu hiyo kushiriki mashindano ya klabu bingwa Taifa, pale ndipo alipopata mchongo na watu mbalimbali ikiwamo aliyekuja kuwa kocha wake, Abdallah Salehe (Comando).

“Tuliporejea Dar es Salaam baada ya mashindano ya 1998, mwaka uliofuatia nilishiriki Mashindano ya Taifa, pale ndipo Kimbau aliniona, alinifuata na kunieleza mipango yake ya kutaka kunichukua, wakati ule nilikuwa bado naishi nyumbani kwa mzee.”

APEWA KAZI YA KUZOA TAKA DAR

Cheka anasema, kabla mipango ya Kimbau kumchukua haijakaa sawa, kuna jirani yao mmoja alimuonea huruma namna alivyokuwa na umri mdogo, lakini anapambana kimaisha.

“Nadhani aliangalia mazingira ya nyumbani jinsi yalivyokuwa magumu, siku moja akaniuliza, ‘nikikutafutia kazi yoyote utafanya?’ Nilikuwa na hali ngumu, wala sikutaka kujiuliza mara mbilimbili, nikamkubalia bila hata kuhoji mshahara wala aina ya kazi ambayo nitaifanya.

“Yule mama aliniambia niende pale Anatoglo, Mnazi Mmoja kuna mzee nionane naye, siku iliyofuata asubuhi saa 12 nilifika pale (Mnazi Mmoja) nikakutana na huyo mzee, nikajitambulisha akaniambia kazi iliyopo ni ya kuzoa taka Manispaa ya Kinondoni.

Cheka anasema, kutokana na hali ngumu aliyokuwa nayo, wala hakujiuliza mara mbili, alianza kazi siku hiyohiyo akiwa na wenzake na wakatakiwa kukusanya taka kwenye Manispaa ya Kinondoni na kwenda kuzimwaga Dampo la Kiembembuzi, Vingunguti, Dar ilikuwa kwa siku kila mmoja amepangiwa kukusanya tripu nne na kituo cha kazi kilikuwa Anatoglo.

NGUMI ZA KULIPWA

Cheka bingwa wa zamani wa dunia anasema, Kimbau ndiye aliyemuingiza kwenye ngumi za kulipwa baada ya kuamua kumchukua yeye na baadhi ya mabondia na kuwalipia chumba na kuwanunulia chakula kwenye kambi yake.

“Nilitoka nyumbani na kwenda kwa Kimbau, tulikuwa tunaishi Sinza, Kimbau alituchukua tulikuwa kama sita hivi, nakumbuka alikuwepo Magoma Shaban, Simba wa Tunduru, Stanley Mabesi na Masudi Kambega, mmoja nimemsahau lengo lilikuwa tujiandae kwa ajili ya kwenda kucheza ngumi Italia.

“Pamoja na kuwa na Kimbau lakini sikuacha kazi ya kuzoa taka, kwenye kibarua changu, muda wa kufika kazini ilikuwa saa 12:00 asubuhi.”

Anasema aliweka utaratibu wa kuwa anatoka Sinza hadi Mnazi Mmoja kila siku saa 11 akikimbia na alifanya hivyo wakati wa kutoka kazini pia.

“Nilifanya hivyo kwa sababu mbili, kwanza kama mazoezi, lakini pia nilikuwa napunguza bajeti ya nauli za kila siku.

“Kuna mzee mmoja pale Mnazi mmoja alipenda namna nilivyokuwa najituma, hivyo akajitolea kila siku kunipa buku (sh 1,000) ya chai, nilifanya kazi kwa juhudi mno, kuna wakati hata Kimbau asipotoa pesa ya matumizi kwenye kambi yetu mimi kupitia fedha ya ujira wa takataka nilikuwa nalisha kambi, ilikuwa ni kazi ambayo ilinipa unafuu wa maisha tofauti na nilivyokuwa kwa mzee,” anasimulia Cheka.

ALIKUTANA MAITI

Cheka anasema, akiwa kwenye kibarua cha kuzoa taka, alikutana na taka za ajabu, kuna wakati alikuta hadi na maiti za watoto wachanga ndani ya taka zikiwa zimetupwa.

“Ilikuwa ni kazi yenye changamoto, kuna wakati unazoa taka lakini unakuta na maiti ya kichanga imeviringishiwa humo. Kwa kuwa ni kazi yetu, basi unakuwa huna namna zaidi ya kuzistiri kwenye mfuko na kuzihifadhi maiti hizo,” anasema Cheka kwa huzuni kidogo na kuendelea.

“Ndiyo, ilikuwa kazi yetu, tukikuta hivyo tunakichukua kitoto tunakistri kwenye mifuko ikiwezekana kukifukia, tunafanya hivyo lakini kwenye kazi hiyo ndiko nilijifunzia kufanya biashara ya kuokota na kuuza chupa.

“Nimekutana na matukio hayo mara nyingi tu, lakini pia kuna wakati kazi inakuwa nzuri, unaweza kuokota fedha kwenye takataka hasa zile za maduka ya Wahindi.

“Hizo fedha nadhani ni wafanyakazi walikuwa wanaiba wanazificha katika takataka, lakini kabla ya kuzichukua, gari letu linapita kuchukua taka zinakuwa bahati yetu.

ALALA MSAMVU WIKI MBILI

Cheka anasema safari ya kwenda kucheza Italia ilishindikana baada ya kuonekana umri wake bado mdogo, hivyo mabondia wenzake waliokuwa kambi akiwamo Stanley Mabesi ndiyo walikwenda, kitendo hicho kilimvuruga na kujikuta hata kazi yake ya kuzoa taka ameipoteza.

“Sikuwa na pa kwenda zaidi ya kurudi nyumbani, ambako kwa kweli sikufikiria tena kurudi kwa mzee, kutokana na maisha ya mama wa kambo yalivyokuwa, hivyo nikajikuta naamua kupanda basi kwenda Morogoro.

“Siku niliyoondoka kwa Kimbau, kuna mtu mmoja wa ngumi anaitwa Spince alimwambia Kimbau, unamuacha huyu ‘dogo’ lakini utakuja kujuta baadaye, kwani kati ya mabondia wake, mimi (Cheka) ndiye niliyekuwa na kipaji cha ngumi.

“Kimbau hakujali, alinipa elfu 20 kama nauli, nirudi nyumbani, nakumbuka ilikuwa mwaka 2000, niliondoka Dar es Salaam na kuelekea Morogoro kwa mara ya kwanza nilikuwa na Sh 20,000 ambayo nilipewa na Kimbau kama matumizi na ndiyo niliitumia kama nauli kuniwezesha kufika huko.”

Bondia huyo anasema, hakuwa na wazo la kumtafuta mama yake ambaye ni raia wa Msumbiji, na mpaka leo hafahamu ni kwa sababu gani hakufikiria kumtafuta mama yake. Huenda ni kutokana na umri wake wakati ule ulikuwa mdogo au changamoto za maisha alizokuwa akizipitia.

“Baada ya kushuka Msamvu, sikuwa na uelekeo, sikujua nitalala wapi, usiku ulipoingia nilijisogeza pembezoni mwa makorido ya maduka yaliyokuwepo stendi, nikatafuta boksi nikatandika chini na kulala.

“Asubuhi kulipokucha, niliamka mapema, ilikuwa saa 10 alfajiri, nilianza kujisogeza kwa kina mama wanaopika chakula maeneo jirani na stendi (mama n’tilie) kuomba vibarua ili niweze kupata kula.

“Sikuona shida sababu wakati nikiwa bado kwa mzee kazi hizo nilizifanya sana, nilipata kibarua cha kuosha vyombo na kuzoa takataka kwa wapika chakula kwenye eneo lile, nilifanya kibarua, ikifika usiku najisogeza kwenye korido la maduka nalala,” anasimulia.

AACHA KULALA STENDI

Cheka anasema siku moja alikutana na mabondia ambao aliwahi kukutana nao kwenye mashindano ya klabu bingwa Taifa ambayo yalifanyika Mwanza. Enzi akiwa na Ngome. “Masela walinichukua tukaenda kuishi maskani, ule ndio ukawa mwanzo wa kuondokana na maisha ya kulala Stendi ya Msamvu, lakini niliendelea na kibarua changu cha kufanya usafi eneo la stendi ambalo liliniingizia kipato kidogo, taratibu nikaanza kuzoea maisha ya Morogoro.

AKUTANA NA COMANDO

Cheka anasema kwa kuwa ngumi ulikuwa ni mchezo ambao aliamini ipo siku ungemtoa kimaisha, licha ya changamoto alizokuwa akipitia, hakuacha kufanya mazoezi.

“Nilianza harakati za kumtafuta Kocha Comando (Abdallah Salehe ambaye ni kocha wake hadi sasa), nilimfahamu wakati alipokuja Mwanza kwenye mashindano ya ngumi akiwa na timu ya Morogoro, mimi nikiwa Ngome.

“Siku nilipofanikiwa kukutana naye, nilimueleza mipango yangu, kocha wala hakuniuliza maswali zaidi, alikubali kunisaidia nikaanza kufanya mazoezi chini yake.

“Siku moja alikuja maskani nilipokuwa nakaa na wale marafiki zangu, kwa kweli kocha hakupenda maisha yale, ndipo akaamua kunichukua nyumbani kwake na kunilea kama mwanawe.

“Hata majirani walikuwa wakiamini mimi ni mmoja kati ya watoto wa Comando, walizoea kuniita mjukuu wa Abdul Salehe ambaye alikuwa baba yake na Kocha Comando.

Unajua baada ya hapo nini kilifuata kwa Cheka, fuatilia kesho Ijumaa ndani ya Mwanaspoti ufahamu mazito zaidi.