Ngorongoro Race wanariadha 1,000 kuondoka na medali

Muktasari:

 

  • Tayari shule zaidi ya tano za jijini Arusha zimethibitisha kupeleka zaidi ya watoto 100 katika mbio hizo mwaka huu, watoto watakimbia umbali wa kilometa 2.5

Dar es Salaam.Kamati ya Maandalizi ya mbio za Ngorongoro (Ngorongoro Race) imepanga kutoa medali kwa wanaridha 1000 wa kwanza watakaomaliza mbio.

Mbio hizo zimepangwa kufanyika Aprili 20 mkoani Manyara.

Mratibu wa Mbio hizo, Meta Petro alisema wameweka utaratibu huo ili kuwapa hamasa washiriki kwenye mbio hizo.

Amesema kuwa medali hizo zinatarajia kutua nchini wakati wowote kuanzia sasa kwa ajili ya mbio zitakazoanzia kwenye lango Kuu ya kuingilia na kutokea katika hifadhi ya Ngorongoro na kumalizikia kwenye viwanja vya Mazingira Bora mjini Karatu.

Amesema msimu huu mbio hizo zitakuwa na msisimko wa aina yake na zawadi zitaongezwa tofauti na zile za mwaka uliopita huku akisisitiza kuwa zitashirikisha wanariadha wengi wandani na nje ya nchi kutokana na uamasishaji ulioufanya.

Alisema kuwa namba kwa wanaotaka kushiriki mbio za kilometa 21 zitatolewa kwa sh 20,000 wakati zile za kujifurahisha za kilometa tano, zenyewe zitatolewa kwa sh 10,000 na watoto watapewa namba baada ya kutoa sh 5,000.

"Tumeamua mwaka huu kutoa namba kwa watoto kwa gharama ya sh 5,000, ili kuwafanya wawe makini na mbio hizo na sio washiriki kwa kujifurahisha tu,".

Amebainisha kuwa tayari shule zaidi ya tano za jijini Arusha zimethibitisha kupeleka zaidi ya watoto 100 katika mbio hizo mwaka huu, ambazo watoto watakimbia umbali wa kilometa 2.5.