Ngoma wala hana mpango

Muktasari:

Donaldo Ngoma ameongeza changamoto iliyopo kikosini kwao inayofanya washindwe kufikia malengo ni majeruhi ambayo yamekuwa yakiwaandama nyota wengi wa timu hiyo ambapo wanashindwa kuunda kikosi imara cha kwanza

Dar es Salaam. Mzimbabwe Donaldo Ngoma juzi kati alifunga bao lake la tano katika Ligi Kuu Bara msimu huu wakati timu yake ya Azam FC ikiizamisha Mwadui FC, lakini straika huyo amefichua kiatu cha dhahabu sio kipaumbele chake kwani kikubwa anachokiangalia ni kuhakikisha timu yake inapata mafanikio.

Mzimbabwe huyo ambaye bao lake hilo liliisaidia timu yake kufikisha pointi 44 katika michezo 19 iliyocheza ilipunguza pengo baina yake na vinara Yanga inayoongoza ikiwa na alama 53.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ngoma alisema nafasi ya kupambania kiatu anayo lakini haipi kipaumbele zaidi ikitokea akafunga mabao mengi, basi atakuwa miongoni mwa nyota wanaowania kiatu hicho.

“Kufunga ndio kazi yangu, hivyo nikisema nitafunga mabao mangapi nitakuwa nadanganya ila kila nikipata nafasi ya kufunga nitafunga na ninataka kufunga idadi kubwa ya mabao ambayo yataisaidia timu yangu.

“Azam ina washambuliaji wengi na wazuri kila mmoja anatamani kufunga lakini sio rahisi kupachika mpira nyavuni kila mmoja, hivyo kuna kumtengenezea mwenzangu ili afunge na kufunga nitapambana katika hali zote kikubwa ni kuona Azam inapata mafanikio,” alisema.

Ngoma aliongeza changamoto iliyopo kikosini kwao inayofanya washindwe kufikia malengo ni majeruhi ambayo yamekuwa yakiwaandama nyota wengi wa timu hiyo ambapo wanashindwa kuunda kikosi imara cha kwanza.