Ngoma hana hamu na Nyoni

Muktasari:

  • Ngoma aliongeza kuwa katika mchezo huo, Nyoni alimnyima kabisa nafasi kwa kumkaba hadi mwisho hivyo, kukosa nafasi ya kupachika bao.

MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Donald Ngoma amekiri muziki wa Simba ni kiboko na kuweka wazi kuwa, beki Erasto Nyoni amemlaza na viatu.

Hayo aliyasema siku moja baada ya timu yake kugawana pointi moja na Simba katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ngoma alisema mchezo ulikuwa mzuri na kuweka wazi kwamba, hali ya uwanja ilikuwa kikwazo kwao kuonyeshana soka maridadi na kuondoka na alama tatu.

“Mchezo ulikuwa mzuri nimefurahia kucheza na timu inayojua soka, lakini uwanja ulikuwa kikwazo kwani maji yalijaa na kutunyima nafasi ya kuonyesha soka safi.

“Simba wapo vizuri kila idara na upande wetu tulijiandaa kwa ushindani kwani, muda mwingi tulishindana kusaka bao ila milango ikawa migumu,” alisema.

Ngoma aliongeza kuwa katika mchezo huo, Nyoni alimnyima kabisa nafasi kwa kumkaba hadi mwisho hivyo, kukosa nafasi ya kupachika bao.

“Tulicheza vizuri ukizingatia tulikutana na timu ambayo inapambana kutetea taji, mchezo ulikuwa mzuri mwalimu atakuwa ameona mapungufu yetu yalikuwa wapi, lakini yule Nyoni ni hatari sana kwa kukaba,” alisema Ngoma.