Ngoma ataka mataji zaidi Azam

Monday January 14 2019

 

By Charity James

Dar es Salaam. Mshambuliaji Donald Ngoma amesema amesajiliwa Azam FC ili kuisaidia timu hiyo kutwaa makombe yote wanayoshiriki na siyo kuongeza idadi ya wachezaji.

Ngoma alisema amefurahi kutwaa ubingwa wa kwanza akiwa katika timu hiyo na anaamini milango bado iko wazi hata kwa ubingwa wa ligi na FA.

Alisema pamoja na kufanikiwa kutwaa ubingwa huo pia mashindano hayo waliyatumia kama mazoezi kujifua kwaajili ya Ligi Kuu na wanaamini yalikuwa na chachu kubwa sana kwao na ndio maana wametwaa ubingwa.

"Mashindano yalikuwa mazuri na ya ushindani japo yalikuwa na muda mdogo wa mapumziko tumerudi sasa tunasahau furaha yote ya ubingwa tunaangalia Ligi na FA ambayo pia malengo yetu ni kuhakikisha tunatwaa ubingwa,"

"Nimecheza michezo yote tofauti na Ligi naamini ndio mwanzo wa mimi kurudi katika fomu yangu ya zamani nilipotua kutoka Zimbabwe japo sio rahisi sana kurudi kutokana na kutoka katika majeruhi narudi mdogomdogo," alisema Ngoma.

Naye nahodha wa Azam FC, Agrey Morris amesema timu yao inanafasi kubwa ya kutwaa mataji mawili msimu huu.

Morris alisema pamoja na kuzidiwa pointi kumi na vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wao wakiwa na mchezo mmoja nyuma yao wanaamini michezo iliyobaki inaweza ikawapa ubingwa huku wakiwaombea wapinzani wao wapoteze.

"Tuna michezo mingi iliyobaki tukiicheza vizuri kwa kupata pointi zote na wenzetu wakapoteza basi nafasi ya sisi kutwaa ubingwa huo ni kubwa sana na tunaamini sio ligi tu hata kombe la FA," alisema Morris.

Advertisement