Ngoma, Nado wapewa rungu

Muktasari:

Hata hivyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat', alisema kwa upande wa uongozi wamekamilisha kila kitu na benchi la ufundi limewahakikishia ushindi na kila mmoja aone hilo ni suala la kitaifa.

MASTAA wa Azam FC, Donald Ngoma na Iddn Seleman 'Nado' ambao kwa muda mrefu walikuwa nje kwenye kikosi hicho kutokana na sababu mbalimbali za kiafya, leo Jumamosi jioni watakuwa kwenye orodha ya Kocha, Etienne Ndayiragije watakapovaana na Fasil Kenema katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho barani Afrika kwenye Uwanja wa Chamazi Complex.
Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Idd alisema pamoja na wachezaji hao, pia Daniel Amoah naye yupo fiti kuwavaa waethiopia hao na wapo tayari kuwapa raha watanzania kuelekea mchezo huo huku wakiomba sapoti ya mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani.
"Ni mchezo ambao tunahitaji ushindi kwa hali na mali na tiketi tayari zimeanza kuuzwa sehemu mbalimbali kama vile Azam Ice Cream, Magomeni Mapipa, Azam Complex na hata kwenye duka letu la vifaa vya michezo zinapatikana tiketi," alisem Idd.
Alisema benchi la ufundi kwa kutambua ugumu na umuhimu wa mchezo huo wamefanya marekebisho kadhaa ya kikosi chao ili kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo, kutokana na makosa ya mchezo uliopita hasa kwa kuwajumuisha wachezaji ambao katika mchezo uliopita hawakucheza.
Hata hivyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat', alisema kwa upande wa uongozi wamekamilisha kila kitu na benchi la ufundi limewahakikishia ushindi na kila mmoja aone hilo ni suala la kitaifa.