Ngoma, Azam wapania Kagame

Muktasari:

Mechi hiyo ya Azam na Meniama walioalikwa kwenye michuano hiyo itapigwa leo Ijumaa baada ya kuing’oa TP Mazembe kwa mabao 2-1, huku wapinzani wao wakiwatupa nje wenyeji APR ya Rwanda kwa mikwaju ya penalti.

UKAME wa mabao, unaomwandama, straika wa Azam FC, Donald Ngoma umezusha maswali mengi kwa wadau wa soka, kwani mpaka michuano ya Kombe la Kagame ikiingia nusu fainali, jamaa kashindwa kutupia hata bao la kuotea na kuzua maswali.

Hata hivyo, nyota huyo wa zamani wa Yanga, amesema mechi dhidi ya Wakongo, AS Meniama ndio itatoa majibu yote kama amefulia ama la kwani amejipanga kuhakikisha anawafunga mdomo wote wanaomponda kwa sasa.

Ngoma aliyeongezewa mkataba wa mwaka mmoja na watetezi hao wa Kagame, ameshindwa kutupia kambani dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo, Bandari Kenya na KCCA Uganda na kufanya mashabiki kudai nafasi yake imeshachukuliwa na Idd Seleman ‘Nado’.

Hata hivyo, straika huyo Mzimbabwe alisema; “Nitazungumza mara baada ya mechi yetu na Meniama, kwa sasa wacha watu wazungumze, ila nitatoa majibu yote uwanjani.”

Mechi hiyo ya Azam na Meniama walioalikwa kwenye michuano hiyo itapigwa leo Ijumaa baada ya kuing’oa TP Mazembe kwa mabao 2-1, huku wapinzani wao wakiwatupa nje wenyeji APR ya Rwanda kwa mikwaju ya penalti.

Kuelekea mchezo huo, Kocha Msaidizi wa Azam, Idd Nassor ‘Cheche’ alisema kila kitu kwao kipo vizuri na anachoshukuru, mpaka sasa mipango yao imekaa vyema na vijana wao wapo tayari kwa vita dhidi ya AS Maniema.

“Tunawafahamu wapinzani wetu tumewafuatilia katika michezo yao tunajua ubora na mapungufu yao na tumejipanga kuhakikisha tunapata ushindi ili kuingia fainali na hatimaye kutetea taji kwa mara ya tatu mfululizo,” alisema Cheche anayemsaidia Kocha Mkuu, Etienne Ndayiragije.