Ngassa aitamani Taifa Stars

Muktasari:

Akizungumza na Mwanaspoti, Ngassa alisema jambo hilo ni la kawaida kwa mchezaji yeyote, hivyo hata yeye anatamani kuitwa tena ili kutoa mchango wake Taifa Stars.

WINGA machachari wa Yanga, Mrisho Ngassa amesema bado ana malengo ya kuitumikia tena timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kwani ana nia na uwezo wa kulisaidia Taifa.
Nyota huyo ambaye aliwahi kuichezea timu hiyo miaka ya nyuma, kwa sasa yupo kambini na timu yake jijini haoa ikijiandaa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco itakayochezwa Septemba 14 mwaka huu uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ngassa alisema jambo hilo ni la kawaida kwa mchezaji yeyote, hivyo hata yeye anatamani kuitwa tena ili kutoa mchango wake Taifa Stars.
Alisema anapambana kuonyesha uwezo wake ili kulishawishi benchi la ufundi la Stars kumuingiza kikosini na kwamba anaamini akiitwa atafanya vizuri.
"Kiukweli hakuna mchezaji asiependa kuichezea timu yake ya Taifa, hata mimi pia bado ninatamani lakini siwezi kuamua tu kuwa nitacheza,nasubiri Kocha akiniita" alisema Ngassa
Hata hivyo, nyota huyo alisema kiwango cha kipa mkongwe, Juma Kaseja kinatokana na kujiamini kwake, kujituma na ndio maana ameaminiwa kuwa na namba ya uhakika.
Kwenye kikosi cha sasa cha  Stars, baadhi ya wachezaji ambao walitamba pamoja na Ngassa ni Kelvin Yondan, Erasto Nyoni na  Agrey Moris ambao wanaaminika kama muhimili wa safu ya ulinzi.