TASWIRA YA MLANGABOY : Ngao ya Jamii: Azam itacheza mpira, Simba itashinda

Muktasari:

Simba, KMC, Yanga, Azam, KMKM na Malindi kila moja ni lazima ipate ushindi ili kusonga mbele na kuendelea kujiweka katika nafasi nzuri ya kuitetea nafasi tuliyopata ya kuwa na timu sita hadi msimu ujao.

Dah! Haikuwa wiki nzuri kwa klabu za Tanzania katika mashindano ya kimataifa baada ya kupata sare nne na kufungwa mechi mbili.

Simba ikiwa ugenini ilipata suluhu kwa UD Songo, Yanga ikiwa nyumbani ikalazimisha sare 1-1 na Township Rollers, KMC ililazimisha suluhu ugenini AS Kigali, Azam ikachapwa 1-0 na Fasil Kenema ugenini, huku KMKM ikachapwa 2-0 dhidi ya Agosto ya Angola mjini Zanzibar wakati Malindi ilitoka sare ya 0-0 dhidi ya Mogadishu City ugenini Somalia.

Natamani nichukue kauli mbiu ya kila mtu ashinde kwao katika mechi za marudiano kwa kuzingatia timu tatu zitakuwa nyumbani, lakini naogopa kuna timu zetu mbili zitakuwa ugenini Yanga na KMKM kwa hiyo hapo mtihani kidogo.

Simba, KMC, Yanga, Azam, KMKM na Malindi kila moja ni lazima ipate ushindi ili kusonga mbele na kuendelea kujiweka katika nafasi nzuri ya kuitetea nafasi tuliyopata ya kuwa na timu sita hadi msimu ujao.

Ukiacha mashindano hayo Agosti 17, 2019, Jumamosi kutakuwa na mchezo wa Ngao ya Jamii itakayowakutanisha mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba na mabingwa wa Kombe la FA, Azam.

Mchezo huu wa Ngao ya Jamii ndiyo unaofungua msimu mpya wa Ligi Kuu na ligi zote za Tanzania Bara, Simba inakwenda katika mchezo huu kwa lengo la kutetea ubingwa wake ilioutwaa msimu uliopita jijini Mwanza kwa kuifunga Mtibwa Sugar kwa mabao 2-1.

Hii itakuwa mechi ya 12 ya Ngao ya Jamii, tangu ilivyoanzishwa mwaka 2001, kisha ikafa na kurudi tena 2009.

Simba inakwenda katika mchezo huo ikiwa na rekodi ya kutwaa taji hilo mara nne, huku Azam pamoja na rekodi yake ya kucheza mara tano mechi hiyo imetwaa mara moja taji hilo.

Taswira imeziangalia Azam na Simba katika michezo yake ya kirafiki pamoja na mashindano ya klabu Afrika yaliyofanyika wiki iliyopita imenifanya niamini Azam itacheza mpira, lakini Simba ina nafasi kubwa ya kushinda mechi hiyo.

Tatizo kubwa la Azam ni mfumo unaotumiwa na kocha Ettienne Ndayiragije umekuwa kikwazo kwake kupata matokeo.

Ndayiragije anaupenda mfumo wa 3-5-1, akiwa amejaza viungo wengi na mshambuliaji mmoja.

Ukiangalia Azam katika mchezo wa fainali Kombe la Kagame dhidi ya KCCA na mechi Kombe la Shirikisho dhidi Fasil Kenema ilitumia mfumo huo imekuwa na matokeo yasiyoridhisha pamoja kutawala mchezo.

Kitendo cha kucheza na mshambuliaji mmoja Obrey Chirwa pekee kinamfanya Mzambia huyo kushindwa kuonyesha uwezo wake hiyo inatokana na viungo wa Azam kuwa mbali naye.

Mfumo 4-5-1 unaifanya Azam kuwa na uwezo mkubwa wa kukaa na mpira katikati, lakini wanakosa ubunifu katika kutegeneza nafasi za mabao wakati wakiwa bize kushambulia wanajisahau kulinda na kufungwa magoli ya kushtukiza.

Aina ya wachezaji wa Kitanzania mfumo wa 4-5-1 umekuwa ni tatizo kwao kuzoea kwa haraka hivyo kocha Ndayiragije anapaswa kurudi katika mfumo wa 4-4-2 au 3–5–2 ni mifumo mizuri kwa kujilinda pamoja na kushambulia.

Changamoto nyingine kwa kocha Ndayiragije naona anajaribu kumtoa Bruce Kangwa kutoka beki na kumpandisha kama winga ni suala zuri kutokana na uwezo wake, lakini Mzimbabwe huyu tatizo lake kubwa ni mpira wake wa mwisho.

Kangwa anaweza kufanya mashambulizi ila krosi zake zimekuwa hazina faida mara nyingi hivyo anahitaji kumtegeneza zaidi katika kutoa pasi za mwisho.

Pia kukosekana kwa Aggrey Morris katika safu ya ulinzi ni pengo analopaswa kulifanyia kazi haraka kama kweli anataka kushinda mechi zake mbili za usoni.

Kwanini naipa Simba nafasi kubwa ya kushinda mchezo huu pamoja na ukweli kuwa mpira ni dakika 90?

Ukiangalia Simba ilivyocheza dhidi ya UD Songo ugenini wamefaidika na kukaa kwao pamoja, jambo linalofanya wacheze kwa kujiamini.

Naamini kocha Aussems ataingia kwa kushambulia kwa kuanzisha washambuliaji wawili katika mfumo wake wa 3-5-2 au 4-4-2, nahodha John Bocco na Meddie Kagere mbele wakisaidiwa na Clatous Chama huku Francis Kahata, Msudani Sharafeldin Shaiboub na Jonas Mkude watakuwa katikati.

Uwezo wa wachezaji moja moja hasa Kagere na makosa ya mabeki wa Azam kunanifanya niamini Simba itashinda mchezo huo.

Kocha Patrick Aussems amefanikiwa kuziba vema mapengo ya nyota wake yaliondoka kwa wachezaji wapya kuzoea haraka mfumo wake.

Pia, Simba inaingia katika mchezo huo ikiwa na rekodi ya kushinda mechi 10 za Ligi Kuu kati mechi 21 walizokutana katika Ligi Kuu tangu Azam FC ipande daraja mwaka 2008. Azam imeshinda mechi tano na kutoka sare sita.

Mwisho wa yote mpira ni dakika 90. Ni hapo tu mshindi wa kweli hupatikana. Tukutane Uwanja wa Taifa Jumamosi.