Neymar mbona analo huko

Wednesday September 16 2020

 

PARIS, UFARANSA. SUPASTAA wa Kibrazili, Neymar huenda akakumbana na kibano cha kufungiwa mechi saba baada ya kutolewa kwa kadi nyekundu kwenye mchezo wa Ligi Kuu Ufaransa dhidi ya Marseille baada ya kumpiga Alvaro.

Neymar alikuwa mmoja wa wachezaji watano waliotolewa kwa kadi nyekundu katika mchezo huo ulioshuhudia Paris Saint-Germain ikikumbana na kipigo cha bao 1-0 nyumbani.

Neymar alimshutumu beki Alvaro kwamba alimfanyia vitendo vya kibaguzi. Lakini, baada ya kutolewa kwa kadi nyekundu kwa kitendo cha kumpiga kinamweka Neymar kwenye hatari ya kufungiwa hadi mechi nane.

Alvaro alijibu tuhuma hizo kwenye ukurasa wake wa Twitter baada ya mechi akiandika ‘hakuna nafasi ya kubaguana’ akaposti na picha akiwa na wachezaji wenzake weusi wanaokipiga kwenye timu moja.

Hata hivyo, PSG wamekaa upande wa mchezaji wao na kutoa taarifa iliyosomeka: “Paris Saint-Germain inamsapoti kwa nguvu zote Neymar Jr ambaye ameripotiwa kulalamikiwa kufanyiwa ubaguzi na mchezaji wa timu pinzani.

“Klabu inataka kusisitiza kwamba hakuna nafasi ya kubaguana kwenye jamii, kwenye soka au kwenye maisha yetu binafsi, hivyo wito kwa kila mtu tuzungumzie hili kuondoa aina zote za ubaguzi duniani.”

Advertisement

Shirikisho la Soka la Ufaransa (LFP) litapitia upya tukio hilo na kujiridhisha kama inapaswa kwa mchezaji Neymar kuongezewa adhabu kutokana na kosa alilofanya.

Advertisement