Neymar asema kitu kuhusu kubaki PSG

Muktasari:

PSG wana uhakika mkubwa wa kumsainisha mkataba mpya Neymar na kubaki kwenye timu yao msimu ujao, lakini jambo hilo litafikia uamuzi kati ya Apri au Mei.

PARIS, UFARANSA . SUPASTAA, Neymar ameripotiwa yupo tayari kusaini mkataba mpya wa kuendelea kubaki Paris Saint-Germain lakini kwa masharti tu kama miamba hiyo itafanikiwa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.

Taarifa hizo ni pigo kwa Barcelona ambao wamekuwa na mchakato wa kumrudisha staa huyo wa Kibrazili kwenye kikosi chao huko Camp Nou.

PSG wana uhakika mkubwa wa kumsainisha mkataba mpya Neymar na kubaki kwenye timu yao msimu ujao, lakini jambo hilo litafikia uamuzi kati ya Apri au Mei.

Kwa mujibu wa ESPN, Neymar mwenye kimo cha futi 5 na inchi 9 anaonekana ametulizana huko Paris, Ufaransa na mambo yake yapo vizuri ndani na nje ya uwanja. Sasa yupo tayari kubaki kwenye timu, lakini kama tu mabingwa hao wa Ufaransa watabeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka huu.

Neymar alisema: “Mipango yangu ni kushinda kila kitu nikiwa nan Paris Saint Germain na timu ya taifa ya Brazil. Kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kubeba Copa America na hapo ndio itakuja kutazama changamoto zingine.”

Kuhusu Ligi ya Mabingwa Ulaya, Neymar alisema: “Tunafahamu tuna kikosi chenye uwezo wa kuwa moja ya timu zitakazofika fainali.”

Mkataba wa Neymar kwenye kikosi hicho umebakiza miaka miwili na nusu na imeripotiwa kumekuwa na mazungumzo baada ya mkurugenzi wa michezo wa PSG, Leonardo na baba yake staa huyo, ambaye ndiye wakala wake.

PSG ilimsajili Neymar kwa ada inayoshikilia rekodi ya dunia kwa sasa ya Pauni 189 milioni akitokea Barcelona miaka miwili iliyopita.