Neymar, Barca ipo hivi

Muktasari:

  • Hatuwezi kuwazungumzia wachezaji wenye mikataba na klabu nyingine, kwa wakati ule aliamua kuachana na Barcelona, basi pale ndipo ulipokoma uhusiano wetu na yeye.”

BARCELONA, HISPANIA.KOCHA Mkuu wa Barcelona, Ernesto Valverde ameamua kufunguka kuhusu ishu ya Neymar kwamba anapiga debe la kutaka kurudi kwenye timu hiyo yenye maskani yake huko Nou Camp.

Kocha Valverde alisema kwanza kitu kama hicho hakipo, kisha jambo jingine ni kwamba Neymar ni mchezaji wa timu nyingine kwa sasa, hivyo si jambo zuri kumzungumzia.

Kocha huyo alisema uamuzi wa Neymar kuachana na Barcelona aliufanya mwenyewe, hakuna aliyemshinikiza kufanya hivyo. Staa huyo wa Kibrazili alikwenda kujiunga na Paris Saint-Germain miaka miwili iliyopita kwa ada iliyoweka rekodi ya dunia ya karibu Pauni 200 milioni.

Lakini, maisha yake yameshindwa kubamba huko Ufaransa na sasa anapiga hesabu za kurudi kwenye La Liga, kwenda kujiunga na timu yake ya zamani. Taarifa za kutoka Hispania zinafichua kwamba baba yake Neymar amekuwa kwenye wakati mgumu na mabosi wa Nou Camp juu ya mpango wa kukamilisha dili hilo la kumrudisha mwanaye Nou Camp.

Lakini, Valverde alisema: “Kwanza kabisa hii sio kesi.

Neymar aliondoka kwa sababu aliamua kufanya hivyo na kuanzia hapo, hatuna kitu cha kuzungumza zaidi.

Hatuwezi kuwazungumzia wachezaji wenye mikataba na klabu nyingine, kwa wakati ule aliamua kuachana na Barcelona, basi pale ndipo ulipokoma uhusiano wetu na yeye.”

Wiki iliyopita kulikuwa na taarifa kwamba Barcelona wamemtuma mmoja wa maskauti wake kwenda kuzungumza na mawakala wa Neymar juu ya mpango wa kumrudisha kwenye kikosi chao.