Neymar : Barcelona yapeleka ofa ya kihuni kwa PSG

Muktasari:

Jumatano kocha wake, Thomas Tuchel alikiri kwamba alifahamu Neymar anataka kuondoka klabuni hapo kabla hata ya kurudi kwao Brazil kujiunga na kikosi cha Brazil ambacho kilitwaa Kombe la Mataifa ya Amerika Kusini hivi karibuni.

PARIS,UFARANSA.BARCELONA wamekuwa wajanja bwana. Wamepeleka ofa ya Pauni 90 milioni kwa PSG kwa ajili ya kumrudisha staa wao wa zamani, Neymar. Lakini hapo hapo ikawapelekea PSG rundo la majina ya mastaa wao na kuwaambia ‘chagueni wawili hapa pia muwachukue’.

Mastaa sita ambao Barcelona inataka kuwatumia kuwatoa chambo kwa ajili ya kumpata Neymar ni pamoja na Philippe Coutinho, Ousmane Dembele, Ivan Rakitic, Nelson Semedo, Malcom na beki wa Kifaransa, Samuel Umtiti.

Inaelewekea PSG inataka zaidi ya Pauni 200 milioni kwa ajili ya staa huyo mwenye umri wa miaka 27 ambaye miaka miwili iliyopita ilimnunua kwa dau la Pauni 198 milioni lililovunja rekodi ya uhamisho wa dunia kutoka hapohapo Nou Camp.

Barcelona haina pesa nyingi ya kutumia baada ya kuilipa Atletico Madrid kiasi cha Pauni 107 milioni kwa ajili ya kumnasa nyota wa kimataifa wa Ufaransa, Antoine Griezmann ambaye ameshaanza mazoezi na timu hiyo.

Hata hivyo, ipo katika moto wa kumrudisha Neymar klabuni hapo baada ya kuona kuna uwezekano wa kurudiana na staa huyo ambaye tayari ameiambia klabu yake ya PSG anataka kuondoka katika dirisha hili la uhamisho.

Jumatano kocha wake, Thomas Tuchel alikiri kwamba alifahamu Neymar anataka kuondoka klabuni hapo kabla hata ya kurudi kwao Brazil kujiunga na kikosi cha Brazil ambacho kilitwaa Kombe la Mataifa ya Amerika Kusini hivi karibuni.

Mkurugenzi wa Ufundi wa PSG, Leonardo wiki iliyopita alisema Neymar anaweza kuondoka kwa mabingwa hao wa Ufaransa kama tu kutakuwa na ofa ambayo itampendeza kila mtu huku akikiri kulikuwa na mawasiliano yasiyo rasmi na Barcelona.

PSG ilijaribu kumshawishi staa huyo abadilishe mawazo yake lakini nyota huyo hakuiambia klabu hiyo mwelekeo wake. Akiwa nchini Brazil hakucheza katika Michuano ya Copa Amerika kwa sababu aliumia kifundo cha mguu katika mechi ya kirafiki dhidi ya Qatar.

Mtangazaji wa Kituo cha Sky Ujerumani, Max Bielefeld juzi Alhamisi alidai wakala wa Neymar ana uhakika dili hilo litapita ingawa kwa sasa bado ni gumu. Bielefeld alisikika akidai: “Anataka kuondoka na Barcelona wanataka kumrudisha kwa nguvu zote.”

Bielefeld pia alidai baba yake Neymar pamoja na wakala wa mchezaji huyo walipaa Jumatano kutoka Brazil mpaka London kwa ajili ya kuzungumza na wawakilishi kutoka katika Klabu za PSG na Barcelona.

Inaeleweka pia kuwa habari kwamba wakala wa Neymar amekuwa katika mazungumzo na Juventus sio za kweli na staa huyo ameelekeza mawazo yake katika kurudi Barcelona ambayo awali alijiunga nayo mwaka 2013 akitokea Santos ya Brazil.

“Suluhisho pekee kwa dirisha hili la uhamisho la sasa ni Neymar na Barcelona,” aliongeza wakala wa Neymar.

Tangu dirisha kubwa lililopita la majira ya joto Neymar ameanza kuhusishwa kurudi Barcelona baada ya kudaiwa kuchoshwa na maisha ya Ufaransa ndani na nje ya uwanja huku akidai Ligi ya Ufaransa haina ushindani mkali.

Neymar ambaye nyota yake katika Klabu ya PSG imefunikwa na kinda, Kylian Mbappe amedaiwa kuchoshwa na mbinu zinazotumiwa na wapinzani kumdhibiti mara kwa mara ambapo amejikuta akiwa majeruhi muda mwingi.

Real Madrid iliwahi kuchomekea kumtaka staa huyo lakini inadaiwa kwamba mawazo yake ameyaelekeza zaidi kurudi Barcelona ambako aliwaacha rafiki zake, Lionel Messi na Luis Suarez ambao aliunda nao utatu mtakatifu klabuni hapo.

Tayari Real Madrid imeachana na mpango wa kumchukua Neymr ambaye awali ilimuona kama mbadala wa muda mrefu wa staa wake wa kimataifa wa Ureno, Cristiano Ronaldo ambey ametimkia Juventus na sasa Madrid imemchukua staa wa kimataifa wa Ubelgiji, Eden Hazard kutoka Chelsea.