Netiboli kuchezwa Uwanja wa Mburahati

Muktasari:

  • Kadewele alisema mpango uliopo ni kuuboresha Uwanja wa Mburahati kwa kujenga majukwaa, kuuwekea nyasi bandia na kujenga viwanja vya michezo mingine ikiwamo netiboli na riadha.

UNAUKUMBUKA ule Uwanja wa Kifa? sasa buana wenyewe wanakwambia sio wa Kifa tena ni Uwanja wa Mburahati Ubungo.

Uwanja huo unapigiwa hesabu ya kuboreshwa na hivi karibuni usishangae kuuona ukiwekewa nyasi bandia, maboresho hayo hayataishia hapo kwani utajengwa hadi uwanja wa netiboli.

“Bajeti ya ukarabati wake imeshaandaliwa na siku si nyingi utekelezaji utaanza,” alisema Ofisa Michezo wa Manispaa ya Ubungo, Fredrick Kadewele wakati akikabidhi vyeti kwa makocha 27 waliohitimu kozi ya awali iliyosimamiwa na Chama cha Soka Ubungo (UFA) na kupewa sapoti na maduka ya Mamu Pharmacy, chini ya bosi wake, Ahmed Presidaa.

Kadewele alisema mpango uliopo ni kuuboresha Uwanja wa Mburahati kwa kujenga majukwaa, kuuwekea nyasi bandia na kujenga viwanja vya michezo mingine ikiwamo netiboli na riadha.

“Tunahitaji Ubungo ipige hatua si kwenye soka tu,michezo yote ifanyike, lakini hayo yatawezekana tukiwa na viwanja, ndiyo sababu tumeamua kuanza na ukarabati wa uwanja wa Mburahati Ubungo,” alisema.

Katibu Mkuu wa UFA, Frank Mchaki alisema ukarabati huo ni mwanzo mzuri wa maendeleo ya michezo kwenye manispaa hiyo ya Ubungo.