Nembo 'Mascot' ya AFCON U17 yazinduliwa Dar

Muktasari:

 

  • Hizi ni fainali za kwanza kubwa za mashindano ya soka barani Afrika kuandaliwa nchini Tanzania

Dar es Salaam. Nembo maalum ya mashindano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 (AFCON U17) imezinduliwa leo saa 5 asubuhi jijini Dar es Salaam.

Hafla ya uzinduzi wa nembo hiyo imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Uwanja wa Taifa jijini chini ya Usimamizi wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe.

Mbali na Dk Mwakyembe, wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Leodegar Tenga, Makamu wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Athuman Nyamlani, Mkurugenzi wa Michezo, Dk Yusuph Singu na Katibu wa BMT, Alex Mkenyenge.

Wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Mwamuzi Mstaafu wa Kimataifa, Leslie Liunda, Wawakilishi wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) pamoja na mashirika mengine, wajumbe wa kamati ya maandalizi ya mashindano hayo pamoja na wanahabari.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa nembo hiyo, Mkurugenzi wa maendeleo ya michezo, Dk. Yusuph Singu alisema kuwa ni ishara rasmi kuwa mashindano hayo yatafanyika nchini.

"Wakaguzi wa CAF walikuja hapa mara mbili na tukawa tunangojea waje kwa mara ya mwisho na wameshafanya hivyo hivyo sasa tuna uhakika kuwa mashindano hayo yatafanyika hapa nchini," alisema Singu