Nduda aipa saluti Ligi ya Wanawake

Muktasari:

  • Aliwataja baadhi ya mastaa katika ligi hiyo kama Mwanahamisi Omary (Simba Queens), Fatuma Mustapha, Asha Rashid (JKT Queens) na Zuena Aziz wa Baobab Queens kwamba ni miongoni mwa wachezaji ambao wapo fiti na wanaweza wakala sahani moja na wanaume.

KIPA wa Ndanda FC, Said Mohamed ‘Nduda’ amesema soka la wanawake linakuwa kwa kasi na kudai wakipatikana wadhamini litakuwa na mvuto kama ilivyo timu za wanaume zinazocheza Ligi Kuu Bara.

Nduda alisema licha ya kutopata muda mwingi wa kufuatilia ligi hiyo kwa sehemu alikiri kuviona vipaji vya hali ya juu alivyodai vinahitaji kupewa motisha ili kufikia malengo yao.

“Ligi Kuu ya Wanaume ina motisha nyingi kama mchezaji bora wa mwezi, ofa za klabu zenyewe na mashabiki kujitokeza kwa wingi kuangalia wanapocheza hayo yakipelekwa kwenye ligi ya wanawake Tanzania kutakuwa na burudani ya aina yake.

“Kwa namna wanavyojua kucheza utadhani ni wanaume, wapo fiti, wanamiliki mipira, mafundi wa kucheza na nyavu kasi ndio usiseme kiukweli kuna haja ya kuwaangalia wanawake kwenye ligi yao baadaye yatakuwepo manufaa,” alisema.

Aliwataja baadhi ya mastaa katika ligi hiyo kama Mwanahamisi Omary (Simba Queens), Fatuma Mustapha, Asha Rashid (JKT Queens) na Zuena Aziz wa Baobab Queens kwamba ni miongoni mwa wachezaji ambao wapo fiti na wanaweza wakala sahani moja na wanaume.

“Unajua kuna wachezaji ukiwatazama unajua hata akicheza na wanaume bado watafanya mambo makubwa mfano hao niliowataja hapo juu,wanajua naamini hata kwenye timu zao ni nguzo,” alisema.