Ndolanga ashindwa kujizuia

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Tanzania (FAT, sasa TFF), Muhidin Ndolanga

Muktasari:

Msimu huu umetafsiri na aliyekuwa mwenyekiti wa FAT (sasa TFF), Muhidin Ndolanga kama utafichua mengi kutoka kwa wachezaji wazawa na wageni, kubwa ikiamini ligi kuu itakuwa na ushindani wa hali ya juu.

MNAMKUMBUKA aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Tanzania (FAT, sasa TFF), Muhidin Ndolanga? Enzi zake bwana, alikuwa na misimamo ambayo wakati mwingine ilimfanya aonekane kama mbabe fulani hivi.

Hata hivyo Ndolanga, anafuatilia soka la Bongo na amecheki idadi ya timu 20 za Ligi Kuu na kuamua kuwapa ukweli nyota wa timu hizo, akidai mwingi wa mechi itakuwa kipimo cha wachezaji hivyo lazima wajipange ili wasiumbuke.

Ndolanga alisema uwepo wa timu nyingi zinafichua ubora na udhaifu wa nyota wazawa na wageni, kujua namna wanavyolichukulia soka, umakini wao pamoja na viwango kama vitastahimili kwa msimu mzima wa 2018/19 ambao una mechi 38.

“Huwezi kufananisha timu 20 na 16 ambazo zilikuwa zinashiriki mwanzo, lazima msimu huu ligi itakuwa bora na pia ni kipimo cha kuwajua wachezaji ambao soka lipo damuni kwao, kwani inawapa nafasi ya kucheza muda mrefu ambapo itawafanya wajengeke kwa uzoefu.

“Lakini kwa wale wajanja wajanja ambao hawakuwa na maandalizi imara basi na wao wataonekana kwa kuchoka mapema, ndio maana nimesema iwafanye wachezaji wajitathimini kama kweli soka ni sehemu ya maisha yao,” alisema Ndolanga.

Aliwataka wazawa wajifunze kwa Mbwana Samatta aliyejijengea jina heshima baada ya kupata nafasi ya kucheza TP Mazembe na sasa Genk ya Ubelgiji, akisisitiza kila nafasi kwao iwe lulu ya kuwafanya wafike mbali.

“Wakitumia vizuri nafasi wanazozipata basi madini yaliopo miguuni kwao, yatawafanya wakue kiuchumi na kufanya wategemewe na taifa, ndugu na chipukizi watakaokuja nyuma yao,” alisema.

Ndolanga, alizungumzia pia Simba na Yanga akidai ikimalizika kwa mzunguko wa kwanza ndipo zitakapoanza kuonyesha makucha yao na kudai kwa sasa ngumu kuzitathimini.