Ndoa ya Kocha Benitez, Mbao FC mbioni kuvunjika

Muktasari:

  • Mbao FC ilikuwa na mwanzo mzuri wa Ligi Kuu ilipokuwa chini ya Kocha Amri Said 'Stam' ambaye aliiacha nafasi ya nne kwenye msimamo na baadaye kutimkia zake Biashara United ya mkoani Mara.

Mwanza. Klabu ya Mbao FC imesema inatarajia kuvunja mkataba na kocha wake Mkuu, Ally Bushiri ‘Benitez’ kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo matokeo yasiyoridhisha kwa timu hiyo.

Benitez alijiunga na timu hiyo Desemba mwaka jana akichukua mikoba ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Amri Said ‘Stam’, ameiongoza mechi 13 na kushinda tatu, sare tatu na kupoteza saba na kuwa nafasi ya 14 kwa alama 36.

Afisa Habari wa Klabu hiyo, Chrisant Malinzi alisema hadi sasa Kocha huyo amewekwa pembeni na timu na kwamba wanasubiri kikao cha leo Jumanne au kesho Jumatano ili kuvunja mkataba naye.

Alisema sababu za kuamua kuachana na kocha huyo ni kutokana na matokeo yasiyoridhisha pamoja na mambo mengine ya nje ya uwanja ambayo kimsingi hayajafurahisha timu.

“Hadi sasa hayupo na timu, amesimamishwa kwa faida ya klabu, tunasubiri kesho Jumanne (leo) au Jumatano (kesho) kukaa naye kumalizana,tatizo kubwa ni matokeo mabovu, timu imeshuka mno,”alisema Malinzi.

Afisa huyo aliongeza kuwa Mbao haitasita kufukuza makocha iwapo haitaridhishwa na mwenendo wa matokeo na kwamba hata klabu zingine zikiwamo za Ulaya hufanya hivyo pale inapobidi.

Benitez alisema yeye ni kocha halali wa Mbao FC na kwamba hajapata taarifa yoyote ya kukalishwa kikao kwa aliji ya kuvunja mkataba.

Alisema kuwa ishu ya kutokuwapo kwenye benchi la ufundi wakati Mbao ikicheza juzi ugenini na Mbeya City, ilikuwa ni matatizo binafsi ambayo hayakumruhusu kuwepo.

“Mimi nipo na timu na ndiye Kocha wa Mbao ni kweli sikuwepo wakati wa mechi na Mbeya City kutokana na matatizo binafsi ila sijaitwa na uongozi kwa sababu zozote,”alisema Benitez.

Kocha huyo aliongeza kuwa iwapo Mbao itaamua kuachana naye hatakuwa na la ziada kwani yeye ni mwajiriwa hivyo maamuzi yoyote atakuwa tayari kuyapokea.