Ndo hivyo, sababu ya Messi kufyumu kuuzwa kwa Suarez

 BARCELONA, HISPANIA. MOJA ya sababu zilizomfanya Lionel Messi kuwaambia mabosi wa Barcelona kwamba anataka kuachana na timu hiyo kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi ni kitendo cha kumwambia Luis Suarez aondoke. Suarez aliachana na Barcelona Jumatano iliyopita akiwa mchezaji namba tatu kwa kufunga mabao mengi kwenye kikosi hicho, ambapo alitumbukiza wavuni mabao 198 katika mechi 283.

Lakini, straika huyo raia wa Uruguay aliambiwa kwenye simu tu na kocha mpya, Ronald Koeman kwamba aondoke tu, hana tena cha maana anachoweza kukifanya Camp Nou.

Jambo hilo la Suarez ilikuwa habari mbaya kwa Messi. Mastaa hao kutoka Amerika Kusini wamekuwa na uhusiano mzuri ndani na nje ya uwanja - hata familia zao zimekuwa na uhusiano wa karibu. Kwa sasa Suarez ni mchezaji wa Atletico Madrid na jambo hilo limemwaachia majonzi Messi kwa sababu ameondoka mchezaji aliyeshirikiana naye kufunga mabao mengi huko Barcelona.

Kwa mujibu wa takwimu za Transfermarkt.com hii hapa orodha ya mastaa waliohusika kwenye mabao mengi waliocheza sambamba na Messi, huku Suarez akishika namba moja.

18.Bojan Krkic (mabao waliyoshirikiana: 11)

Staa Bojan bahati mbaya alishindwa kutamba na kuendana na sifa aliyokuwa akipewa alipoibukia Barcelona. Bojan aliyedaiwa kuwa ni Messi mpya alicheza na Messi na wawili hao kuhusika na mabao 11.

17.Adriano (mabao waliyoshirikiana: 11)

Messi amekuwa na kawaida ya kupiga pasi za kupenyeza kwa mabeki wa pembeni na hilo linamfanya Adriano kuingia kwenye orodha ya mabeki walioshirikiana na Muargentina huyo. Katika mechi walizocheza pamoja wameshirikiana kwenye mabao 11.

16.Cristian Tello (mabao waliyoshirikiana: 13)

Cristian Tello alicheza mechi 63 sambamba na Messi huko Barcelona, lakini walishirikiana kwenye mabao 13. Tello alitendea haki kila fursa aliyopata kuwa kwenye timu.

15.Gerard Pique (mabao waliyoshirikiana: 15)

Gerard Pique ni beki wa kati na Messi ni mshambuliaji. Lakini, wachezaji hao wameshirikiana kwenye mabao 15 kuifungia timu yao ya Barcelona katika mechi zaidi ya 483 walizocheza pamoja. Kwenye orodha ya mastaa waliocheza mechi nyingi na Messi, Pique ni mmoja wao na bado idadi hiyo itaongezeka zaidi kwa kuwa pamoja.

14.Thierry Henry (mabao waliyoshirikiana: 16)

Baada ya kutua Barcelona akitokea Arsenal, supastaa Thierry Henry alikwenda kukutana na Messi na kucheza pamoja kwenye mechi 89. Katika mechi hizo Henry na Messi walishirikiana kwenye mabao 16 kuifungia timu yao ya Barcelona ili kushinda mechi zake mbalimbali katika La Liga na michuano mingine ikiwamo ya Ligi ya Mabingwa.

13.Sergio Busquets (mabao waliyoshirikiana: 18)

Hakuna mchezaji aliyecheza mechi nyingi na Messi kuzidi kiungo Sergio Busquets. Wawili hao wamecheza zaidi ya mechi 523 na bado wanaendelea kwa sababu bado wapo pamoja. Katika mechi walizocheza pamoja, wawili hao walishirikiana kwenye mechi 18 kuisaidia timu yao kushinda mechi zake. Busquets anacheza kiungo ya chini.

12.Samuel Eto’o (mabao waliyoshirikiana: 23)

Straika Samuel Eto’o, Ronaldinho na Messi ulikuwa utatu matata sana kwenye kikosi cha Barcelona

iliyokuwa ikinolewa na Frank Rijkaard. Hakika wachezaji hao walivutia sana kuwatazama. Eto’o na Messi walicheza pamoja kwenye mechi 105 na kushirikiana katika mabao 23 kuisaidia timu hiyo kushinda mechi zake huko Hispania.

11.Alexis Sanchez (mabao waliyoshirikiana: 24)

Staa Alexis Sanchez hakuwa na wakati mzuri alipotua Manchester United akitokea Arsenal na hivyo kutolewa kwa mkopo kabla ya kuuzwa jumla Inter Milan. Kabla ya hapo, Sanchez alikuwa Barcelona mahali ambako alipata nafasi ya kucheza na Messi kwenye mechi 117 na kuhusika katika mabao 24 wakiifungia Barcelona.

10.David Villa (mabao waliyoshirikiana: 26)

Mshambuliaji David Villa na Messi walicheza pamoja kuitumikia Barcelona katika mechi 102 na mambo yao ya ndani ya uwanja hayakuwa mzaha, wakishirikiana kwenye mabao 26 ikiwa ni wastani wa bao moja katika kila baada ya mechi nne. Baadaye, Villa aliondoka kwenye kikosi hicho na kwenda Atletico kama alivyofanya Suarez.

9.Cesc Fabregas (mabao waliyoshirikiana: 26)

Kiungo Cesc Fabregas na Messi walikuwa pamoja kwenye kikosi cha Barcelona tangu wakiwa watoto na hata familia zao zimekuwa karibu sana. Wawili hao wamekuwa na uhusiano mzuri ndani na nje ya uwanja kwa nyakati zao walizokuwa pamoja Camp Nou. Maswahiba hao kwenye mechi walizocheza pamoja wameshirikiana kwenye mabao 26.

8.Ivan Rakitic (mabao waliyoshirikiana: 27)

Kiungo Ivan Rakitic ni moja ya wachezaji walioachana na Barcelona kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi. Mkali huyo wa Croatia amerudi zake Sevilla, huku akikiri kwamba Messi hakuna rafiki yake wa karibu. Hata hivyo, bado wawili hao walihusika kwenye mabao 27 katika mechi 277 walizocheza pamoja kuisaidia Barcelona.

7.Jordi Alba (mabao waliyoshirikiana: 29)

Kama ingekuwa inahusishwa pasi ya pili kabla ya ile ya mwisho, basi beki Jordi Alba angekuwa anaongoza kwenye orodha ya wachezaji walioanzisha mashambulizi mengi ya mabao ya Messi. Hata hivyo, beki huyo wa kushoto bado amekuwa na mchango mkubwa ambapo na Messi wameshirikiana kwenye mabao 29 walioifungia Barcelona.

6.Xavi (mabao waliyoshirikiana: 43)

Kiungo mwenye pasi zake. Xavi alikuwa mtu na nusu kwenye kikosi cha Barcelona kutokana na namna alivyokuwa akiishikilia safu ya kiungo kufanya mipango kwenda sawa. Kwenye chama hilo la Nou Camp, Xavi na Messi walicheza pamoja mechi 399 na kushirikiana kwenye mabao 43 kuifanya timu yao kushinda kwenye mechi kibao.

5.Dani Alves (mabao waliyoshirikiana: 47)

Beki wa Kibrazili, Dani Alves alipokuwa Barcelona, mara zote kwenye mazoezini ya kupasha misuli moto kabla ya mechi alikuwa akifanya sambamba na Messi na jambo hilo lilikuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki. Wakicheza upande mmoja wa kulia mara nyingi, Messi na Alves walishirikiana vyema uwanjani wakichangia timu yao mabao 47.

4.Pedro (mabao waliyoshirikiana: 50)

Baada ya kutamba kwenye kikosi cha Barcelona, fowadi wa Kihispaniola, Pedro aliondoka kwenda kujiunga na Chelsea - mahali ambako alicheza soka la kiwango cha juu na kubeba mataji. Akiwa Barcelona, alicheza na Messi mechi 270 na wawili hao walishirikiana vyema kuichangia timu yao mabao 50 na kuifanya Barcelona itambe.

3.Andres Iniesta (mabao waliyoshirikiana: 54)

Kiungo fundi wa mpira, Mhispaniola Andres Iniesta alikuwa moto kwelikweli alipokuwa kwenye kikosi cha Barvelona, mahali ambako alicheza mechi kibao sambamba na mkali wa Kiargentina, Messi. Wawili hao walicheza pamoja kwenye mechi 489 huku ushirikiano wao ukizalisha mabao 54 hilo likithibitisha wawili hao kuelewana.

2.Neymar (mabao waliyoshirikiana: 56)

Supastaa wa Kibrazili, Neymar - ambaye ni mchezaji ghali kabisa duniani kwa sasa amecheza mechi 161 pamoja na Messi kwenye kikosi cha Barcelona. Katika mechi hizo, wawili hao walishirikiana kufunga mabao 56 na hivyo kuwa moja ya pacha iliyotengeneza mabao mengi kwenye kikosi cha Barcelona walipocheza pamoja.

1.Luis Suarez (mabao waliyoshirikiana: 96)

Kwenye hili, unaweza kuona kwanini Messi ameumizwa sana na kitendo cha Barcelona kumruhusu Luis Suarez kuondoka kwenye kikosi cha Barcelona. Uhusiano wao wa ndani ya uwanja baina ya wawili hao, umezalisha mabao 96, Suarez akishiriki kwenye mabao mengi zaidi alipocheza na supastaa huyo wa Kiargentina.