Ndio! Gia ndogo ilivyoimaliza Taifa Stars Praia

Muktasari:

Tanzania inahitaji kushinda katika mchezo wa kesho dhidi ya Cape Verde ili kufufua matumaini yake ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Afcon2019 nchini Cameroon

NILIKUWEPO Praia, mji mkuu wa Cape Verde. Taifa Stars ilikuwa nyuma kwa mabao mawili ndani ya dakika 18 tu za mwanzo. Ilishangaza sana. watu wote waliosafiri na timu kwenda Praia hawakutarajia hata sare. Walitarajia Stars ishinde.

Mpaka sasa hakuna majibu ya msingi ya swali kwanini Taifa Stars walipoteza mechi ile? Kuna majibu tofauti. Jibu la kwanza linaanzia katika ukweli wa namna ambavyo mabao yenyewe yaliingia katika dakika za mwanzo.

Wachezaji wa Stars walianza katika gia ndogo. Walianza mechi taratibu na labda walikuwa wamejiamini kwamba wanaenda kushinda mechi. Bao la kwanza liliwachukua kwa mshtuko. Kabla hawajatulia sana wakafungwa bao la pili.

Swali la kwanza ni namna ambavyo Stars hawakutumia mbinu zao zile zile walizotumia mechi dhidi ya Uganda. Katika mechi hii alibadilika mchezaji mmoja tu. Himid Mao. Yeye ndiye hakuanza mechi dhidi ya Uganda lakini kwa ujumla timu ilikuwa vile vile.

Kwanini tuliwadharau sana Cape Verde? Sijui. Katika mechi dhidi ya Uganda tulijua ukali wa Waganda. Wachezaji wetu wakacheza nyuma zaidi huku wakiwa wameubana uwanja. Katika pambano hili hakutuubana uwanja na kufanya mashambulizi ya kushtukiza. Tulitaka kupishana nao kuanzia dakika ya kwanza.

Hata kama tulijiamini lakini tulipaswa kutulia katika lango letu walau kwa dakika 10 na kupima upepo wa mechi. Hatukufanya hivyo. Tulicheza kama tupo nyumbani. Bao lao la pili lilimuacha mpira krosi akiwa peke yake na Himid Mao katika upande wa kulia. Alikuwa wapi Hassan Kessy? Alikuwa wapi mlinzi mmoja wa kati kuja kumsaidia Himid akitokea katikati?

Mechi dhidi ya Uganda hatukucheza hivi. Na ndio maana pia jamaa walitawala katikati kwa sababu kulikuwa na pengo kubwa kati ya walinzi wa kati na Himid. Lakini pia kati ya Himid na wachezaji wa mbele. Waganda hatukuwapa nafasi hii.

Zaidi ya yote karibu kila mchezaji alikuwa ovyo uwanja. Mbwana Samatta alionekana kujitutumua lakini akajikuta akichezesha timu zaidi kuliko kuwa na madhara katika lango la Cape Verde. Simon Msuva hakuwa na siku nzuri. Thomas Ulimwengu hakuwa na siku nzuri.

Alipoingia Shomari Kapombe Stars ilibadilika kidogo kwa sababu alikwenda kucheza eneo la katikati na kuisukuma timu mbele zaidi. Walau eneo la katikati lilipata uhai. Nina uhakika Emmanuel Amunike ataanza naye katika pambano la kesho jioni.

Timu ilibadilika zaidi katika kipindi cha pili na iliingia na gia ambayo walipaswa kuingia nayo katika kipindi cha kwanza. Wachezaji walirudisha mawazo uwanjani na alipoingia John Bocco ilionekana kama vile Stars imerudisha uhai.

Kilichotokea Cape Verde kinaonyesha kwamba kocha Amunike amemaliza fungate lake na mashabik wa soka nchini. Lawama zimeanza na kelele zimeingia mjini. Tumerudi katika maisha ya lawama ambayo yote yanaweza kukoma kesho jioni kama Stars ikishinda.

Katika hali ya kawaida sio haki. Ni mechi moja tu ambayo tumepoteza. Haikuwa siku nzuri kwa ujumla wake. Argentina ufungwa, Ujerumani ufungwa, Brazil ufungwa. Saa 24 baada ya kipigo cha Stars Ujerumani walikuwa wakichapwa mabao 3-0 na Uholanzi ambayo kwa sasa ni kama vile imepotea kisoka.

Kipigo dhidi ya Cape Verde ni kengele tosha kwa Amunike na wachezaji wake. hapana shaka kwa sasa wachezaji wengi watajua kwamba hawapo salama sana katika timu kama wanavyodhania. Kuna wachezaji wenye majina makubwa wanaweza kuwekwa nje muda wowote kuanzia sasa.

Amunike anaweza kuanza kuchukua maamuzi magumu muda wowote kuanzia sasa kwa sababu bado ana nafasi ya kufanya vizuri na timu ikaenda Afcon mwakani pale Cameroon. Ni jambo ambalo linawezekana kwa asilimia nyingi baada ya Uganda kuichapa Lesotho pale Kampala.

Kitu cha msingi ni kushinda mechi ya kesho. Ni kitu kinachowezekana kwa asilimia nyingi. Cape Verde sio timu tishio sana. wachezaji wake hawana nidhamu sana ya ushindi na wangeweza kushinda mabao mengi zaidi kama wangekuwa na nidhamu ya ushindi.

Kwa mtazamo wangu, ushindi wa Cape Verde ulitokana zaidi na uzembe wa Stars kuliko uhodari wao. Kama Stars wakicheza kama walivyocheza dhidi ya Uganda ugenini, kwa kutoa kila walichonacho, basi Stars wanaweza kushinda dhidi ya Cape kesho na pia dhidi ya Lesotho ugenini.

Jambo la msingi ni ile ile ambalo naamini lilitukwamisha Praia. Tuanze kwa gia kubwa. Na kwa sababu mashabiki watakuwa wengi nyuma yetu, kuna uwezekano mkubwa tukashinda mechi. Tatizo kubwa Watanzania wanapenda kuwazungumzia wachezaji ambao hawapoo katika kikosi kama vile ndio ambao wanashikilia maajabu ya Stars.

Hapana. Stars inahitaji kwanza kuwa na siku nzuri kwa wachezaji waliopo. Kuna mtu ambaye anaweza kubadilisha matokeo zaidi ya Mbwana Samatta? Sioni sana. lakini kuna mtu anakwambia kwa sababu Ibrahim Ajibu hakuwepo. Kwa sababu Shiza KIchuya hakuwepo. Kama wao wangekuwepo halafu Samatta na Msuva wakakosekana tungesema kwamba timu imefungwa kwa sababu Samatta na Msuva hawapo.