Ndinga wanazotesa nazo mastaa wa soka mtaani ni balaa tupu

Muktasari:

Staa wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang ni mmoja kati ya wakali wanaopenda kuwa na magari mapya sambamba na Cristiano Ronaldo wa Juventus. Haya hapa ndio magari mapya yaliyoonekana yakiendeshwa na mastaa wa soka kwenye Ligi Kuu England na wengineo mwaka huu.

LONDON, ENGLAND.KILA mwaka, wanasoka wamekuwa wakionyesha jeuri ya pesa walizokuwa nazo kwa kununua magari mapya kutesea mitaani.

Mwaka huu, mastaa kibao wa Ligi Kuu England walionekana ndani ya ndinga mpya wakienda nazo mazoezini, wengine kwenye viwanja kucheki mechi na kipindi kingine kwenda kwenye mitoko yao binafsi kufanya manunuzi ya mambo mbalimbali.

Staa wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang ni mmoja kati ya wakali wanaopenda kuwa na magari mapya sambamba na Cristiano Ronaldo wa Juventus. Haya hapa ndio magari mapya yaliyoonekana yakiendeshwa na mastaa wa soka kwenye Ligi Kuu England na wengineo mwaka huu.

9. Bentley Bentayga Onyx - Pauni 162,700

Wakati ndinga ya Bentayga ilipoingia tu sokoni, haraka sana ikawa gari ya wanasoka kutokana na ilivyo ya kistarehe sana na ukubwa wake. Supastaa wa Manchester City, Raheem Sterling ni mmoja kati ya wakali wanaoendeesha ndinga hiyo sambamba mchezaji wenzake wa huko Etihad, Sergio Aguero. Hivi karibuni pia alionekana staa wa Manchester United, Jesse Lingard akienda nayo mazoezini.

8. Maserati Grancabrio - Pauni 106,285

Hii ni moja kati ya magari mengi yainayomilikiwa na staa wa Juventus na Ureno, Cristiano Ronaldo kwenye maegesho yake. Imetengenezwa katika mwonekano bora kabisa na kuwa moja ya ndinga matata za aina ya Maserati. Kichaa wa magari Ronaldo hakutaka kupitwa na ndinga hiyo ya Kitaliano yenye milango minne ikiwa ni mara ya kwanza Maserati kutengeneza gari ya aina hiyo.

7. Range Rover Autobiography - Pauni 101,260

Moja ya Range Rover matata zinazotesa mitaani na kumilikiwa na wanasoka hasa wa Ligi Kuu England. Kubwa linalowafanya wanasoka kukimbilia gari hiyo ni kutokana na kuwa ya kustarehe sana unapoendeesha.

Michael Carrick, Marcus Rashford, Phil Jones na Harry Kane ni baadhi ya wanasoka wanaomiliki ndinga hiyo ya kijanja mtaani.

6. Lamborghinni Huracan Spyder - Pauni 198,876

Sifa moja wapo ya ndinga hii ni kuwa na spidi ya ajabu inapokuwa barabarani. Huracan Spyder ni gari ya kijanja na ambayo pia bei yake ni ya kijanja pia. Wanasoka kadhaa wamekuwa wakimiliki ndinga hiyo na mmoja wao ni staa ananyesakwa na Manchester United, Mauro Icardi, ambaye ni straika wa Inter Milan ya huko Italia.

5. Ferrari 488 Spider - Pauni 217,219

Straika Mtaliano, Mario Balotelli ni mmoja kati ya wanasoka wa nguvu wanaomiliki 488 Spider. Alikuwa akionekana nayo kwenye mitaa ya huko Italia, anakokipiga kwa sasa tangu akiwa Nice na baadaye kuhamia kwenye kikosi cha Olympique Marseille. Straika wa Man City, Sergio Aguero aliwahi kukodisha ndinga hiyo alipokuwa zake huko Marekani kwenye mapumziko.

4. Audi RS6 Avant - Pauni 80,000

Aud ni gari yenye kasi sana na ni moja ya gari ambazo bei yake imechanganya pia. Ni gari yenye siti tano na ndio maana wanasoka mbalimbali wamekuwa wakizipenda gari hizo kwa ajili ya mitoko yao ya pamoja au na familia zao. Kuna orodha ya wanasoka wengi sana wanaomiliki ndinga hiyo ya kijanja.

3. Mercedes-Benz G-Class - Pauni 91,215

Inafahamika pia kama G-Wagen, Mercedes wamekuwa wakizifanyia marekebisho makubwa gari zao ili kuzifanya kuwa za starehe zaidi. Staa wa Arsenal, Mesut Ozil ni mmoja kati ya wanasoka wanaomiliki ndinga hiyo yeye yake ikiwa ya kijani, huku mwanasoka mwingine aliyevutika na gari hiyo ni Raheem Sterling wa Man City.

2. Bentley Continental GT - Pauni 159,900

Vya zamani siku zote ni vizuri. Ndinga hiyo imekuwa ikipendwa sana na wanasoka na pengine karibu kila mmoja atakuwa nayo. Continental GT mara ya kwanza ilitoka mwaka 2003 na tangu wakati huo imekuwa ndinga maarufu ikionekana mitaani ikiendeeshwa na mastaa kibao. Kikubwa ni mwonekano wake na spidi ndicho kitu kinachowavutia zaidi wanasoka.

1. Range Rover Sport SVR - Pauni 99,620

Ni gari iliyoonekana na mastaa wengi sana wakiendeesha mwaka huu. Wanasoka wengi walionekana kupendezwa na gari hiyo na kuonekana nayo mitaani akiwamo supastaa wa Manchester United, Jesse Lingard. Ni gari ya kijanja sana ambapo thamani yake ya juu imedaiwa kuwa ni Pauni 100,000.