Ndayiragije atimkia Burundi aikacha Mbao

Sunday April 15 2018

 

By Saddam Sadick

Mwanza. Kocha Mkuu wa Mbao FC, Ettiene Ndayiragije ameendelea kukosekana katika mechi za timu hiyo, huku taarifa kutoka ndani ya klabu zikieleza kuwa tayari ameondoka nchini.

Mechi ya mwisho Ndayiragije kuongoza kikosi, ilikuwa dhidi ya Lipuli waliomaliza kwa suluhu ambapo alikumbana na kasheshe ya mashabiki waliomjia juu wakimtaka aachie timu kutokana na matokeo yasiyoridhisha na kusaidiwa na askari polisi waliomtoa uwanjani kwa ulinzi mkali.

Hata katika mchezo uliopita dhidi ya Njombe, Kocha Msaidizi Ahmad Ally ndiye alisimamia, ambapo kwenye mazoezi tangu juzi yanasimamiwa na Kocha mpya, Novatus Fulgence akisaidiwa na Meneja, Faraji Muya ambapo hata leo wawili hao ndio walionekana katika Benchi la Ufundi.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya timu kimesema kuwa Ndayiragije ameshaondoka kwao Burundi tangu jana, huku wakisubiri msimamo wake kama ataendelea kuinoa timu au la.

"Ameondoka kwao Burundi, sisi hatujavunja mkataba naye, tunasubiri kuona msimamo wake,tutapambana kuinusuru timu kutoshuka daraja" kimeeleza chanzo hicho.