Ndayigarije anataka mabao tu

KOCHA wa timu ya Taifa 'Taifa Stars' Ettiene Ndayiragije ni kama amepanga kujilipua katika mchezo wa kesho Jumapili dhidi ya Burundi.
Katika mchezo huo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia, Ndayiragije ameonekana kuwa ataingia na aina ya soka la kushambulia zaidi ili timu yake ivune mabao ya kutosha.
Hali hiyo imejionyesha katika mazoezi ya mwisho ya Taifa Stars kwa  jinsi aina ya kikosi alichopanga.
Kutokana na mazoezi ya mwisho leo Jumamosi yaliyofanyika jioni kwenye Uwanja wa Taifa Ndayiragije alipanga kikosi chenye wachezaji wengi ambao ni washambuliaji tofauti na mchezo wa kwanza uliofanyika Burundi ambao ukimalizika kwa sare ya bao 1-1.
Kikosi ambacho Ndayiragije anatarajia kukianzisha kesho ni Juma Kaseja, Hassan Kessy, Mohammed Hussein'Tshabalala', Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Iddi Seleman Nado, Salum Abubakary, Mbwana Samatta, Simon Msuva na Hassan Dilunga.
Katika mazoezi hayo Ndayiragije alikuwa akidili na mabeki wa pembeni Kessy na Tshabalala akiwataka kushambulia kwa haraka na kupiga krosi zinazotua kwa washambuliaji Samatta, Msuva na Nado.