Ndanda yakataa utamaduni wa Simba, Yanga ijinusuru Ligi Kuu

Muktasari:

Klabu ya Mbeya City na Ndanda FC kwa pamoja zilipanda daraja mwaka 2014.

Mtwara. Klabu ya Ndanda FC ya mkoani Mtwara imezindua kampeni yake ijulikanayo kama ‘Twenzetu Mbeya’ kwa lengo la kuhamasisha mshikamano ili kujinyakulia alama tatu katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya huku ikijiwekea mikakati kuepuka siasa za Simba na Yanga.

Machi 3 mwaka huu, Ndanda FC wanakuchele wanatarajia kucheza na Mbeya City na ndio lengo la kuanzishwa kampeni hiyo baada ya kampeni ya awali kuonyesha matokeo chanya na kushinda michezo mitatu mfululizo katika uwanja wa nyumbani, Nangwanda Sijaona.

Msemaji wa klabu hiyo Idrissa Bandali amesema walianza na kampeni ya kwanza ambayo iliwapa usindi kwa pointi tatu mfululizo.

“Twenzetu Mbeya ina vitu vingi ndani, kwa maana tunataka tuone umoja ule ukiendelea kuwepo, muamko wa wachezaji ukiendelea kuongezeka kwa kiasi kikubwa sana, lakini kitu kikubwa tunachikihitaji ni pointi tatu kwenye uwanja wa Sokoine tutakapocheza na Mbeya City,”amesema

Bandali Ndanda kwa sasa wenye jumla ya alama 32 wanazidi kuwafanya mashabiki wake kuwa na imani nao na kuondoka katika mstari mwekundu lakini kuhakikisha wanamaliza ligi wakiwa katika nafasi nzuri.

“Hatutaki tuwe kama miaka mingine iliyopita bado mechi mbili za mwisho ndipo tunaanza kushikana tunaangalia tunanusurika na kubaki kwenye ligi.

Tunachoamini sisi ni Ndanda kwanza mambo mengine badaye, sijui siasa, Simba na Yanga hatutaki,”amesema Ally Maguna.

“Hatutaki tuwe tena ni wale watu tunaochungulia tundu la sindano na ndio maana tunajitahidi kuhakikisha timu zinazobaki ni pamoja na Ndanda,”amesema Omary.