Ndailagije ashikiria hatma ya Chirwa Azam

Muktasari:

Taarifa zinadai Chirwa amegoma kusaini mkataba mpya na Azam kwa lengo la kutaka kujiunga na mabingwa wateule wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba

Dar es Salaam. Kocha wa KMC, Etienne Ndayiragije anamaliza mkataba wake na klabu hiyo na sasa anahusishwa kutua Azam FC na kushika hatma ya Obrey Chirwa kuendelea kusalia kikosini hapo.

Hivi karibuni iliripotiwa mshambuliaji huyo aliyejiunga na Azam FC dirisha dogo la usajili aligoma kuongeza mkataba mpya na kuhushwa kutua Simba FC.

Chanzo cha ndani kutoka katika klabu hiyo kimeliambia Mwanaspoti.co.tz kuwa kuna uwezekano mkubwa wa Chirwa kushindwa kuongezwa mkataba kutokana na Mrundi huyo kuuambia uongozi kuwa atajiunga na klabu hiyo pamoja na nyota wake.

"Ndailagije ameuambia uongozi anautaratibu wa kusajili nyota wake mwenyewe ili ata ikija ikatokea akashindwa kufikia malengo aliyojiwekea anapaswa kulaumiwa yeye na sio kukuta kikosi kilichosajiliwa hivyo kuwapa mtihani viongozi kutokana na kuongeza baadhi ya nyota mikataba mipya," kilisema chanzo hicho.

Alipotafutwa Meneja wa klabu ya Azam FC, Philip Alando kuzungumzia suala hilo alisema kuwa taarifa hizo hazina ukweli wowote kwa sababu makubaliano ya klabu na mchezaji huyo ni kufanya mazungumzo mara baada ya mkataba kumalizika.

"Tunaheshimu makubaliano na siku zote tumekuwa katika misingi hiyo, mfano hivi karibuni kulikuwa na taarifa kuwa Yakuby anakwenda Simba lakini mwisho wa siku akasaini hadharani na Azam FC na kila mtu aliona hivyo ata suala la Chirwa linahitaji muda," alisema Alando.

"Dirisha dogo tuliingiza wachezaji wawili wa kigeni, Chirwa na Stephen Kingu Mpondo lakini sioni mtu akimuulizia. Pia mkumbuke usajili haufanywi na uongozi, usajili unafanywa na makocha halafu viongozi kazi yao ni kukamilisha tu", ameongeza.

Siku za karibuni zilienea taarifa kuwa Chirwa amegoma kusaini mkataba mpya na klabu hiyo huku zikieleza zaidi kuwa yuko mbioni kujiunga na mabingwa wateule wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba.